NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kipindi hiki ambapo Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wito wa maadili, mshikamano, na amani umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya TANTRADE, Oscar Kissanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Video Albamu ya Kwaya ya Imani ya Mwenge Christian Centre (MCC) jijini Dar es Salaam, Kissanga alisisitiza wajibu wa taasisi za dini kusimama kama nguzo ya maadili, haki na amani katika kipindi hiki muhimu cha demokrasia ya nchi.
“Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, tunahitaji zaidi ya wakati mwingine wowote mshikamano wa kitaifa, uadilifu, na maombi ya dhati. Kanisa na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuhakikisha jamii inabaki kwenye misingi ya haki, amani na upendo,” alisema.
Katika hotuba hiyo, Kissanga aliipongeza Kwaya ya Imani kwa mchango wao wa kiroho kupitia muziki wa Injili, akieleza kuwa kazi zao si tu burudani bali ni faraja kwa jamii na chombo muhimu cha uinjilisti.
Kissanga aliahidi kuchangia Sh. Milioni 10 katika kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa gari aina ya Costa kwa matumizi ya kwaya hiyo, na kuwaalika wadau wengine kuunga mkono juhudi hiyo ya kiroho na kijamii.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wote na watanzania kwa ujumla kujiunga na TCCIA ili kunufaika na fursa za kibiashara,viwanda na kilimo zinazotolewa, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masoko, taarifa za kibiashara, na kuunganishwa na wawekezaji wa kimataifa.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Kanisa la TAG Mwenge Christian Centre na kuhudhuriwa na viongozi wa dini, serikali, wadau wa muziki wa Injili na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.