NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai hadi Septemba 2025), imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 8.97 sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 8.44.
TRA imesema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na kiasi cha Sh. Trilioni 7.79 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/2025.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 2,2025 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema makusanyo hayo yaliyokusanywa kwenye robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai – Septemba 2025) ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na kiasi cha Sh. Trilioni 4.40 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho toka Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka wa fedha 2020/2021.
Amesema wastani wa makusanyo kwa mwezi pia umeongezeka toka kiasi cha Sh.Trilioni 1.47 kwa mwezi mwaka 2021/2022 mpaka kufikia kiasi cha Sh. Trilioni 2.99 kwa mwezi kwa mwaka 2025/2026.
“Kipekee, kwa mara ya kwanza Mamlaka ya Mapato Tanzania imeweza kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 3.47 kwa mwezi mmoja wa tisa ambacho ni kiasi kikubwa kuliko miezi mingine ya nyuma kama hiyo,” amesema Mwenda
Hata hivyo amesema ufanisi huo katika makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 umechagizwa na kuendelea kuboresha mahusiano na walipakodi nchini, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa maelekezo ya Rais Samia ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini bila uonevu.
Amesema TRA imeendelea kuboresha mahusiano na ushirikiano na Wizara, Taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuhakikisha wote wanashiriki katika uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari nchini.
“Mafanikio haya yamechagizwa pia na kuongezeka kwa uwajibikaji wa ulipaji kodi wa hiari miongoni wa walipakodi. Kwa muktadha huu, TRA tunawashukuru sana walipakodi wote. Pia Kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na sera nzuri za uchumi na mazingira ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita kumechangia mafanikio haya,” amesema
Amesema vitu vingine vilivyochangia mafanikio hayo ni matokeo chanya ya uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini kupitia kwa uanzishwaji wa “Dawati la Uwezeshaji Biashara” nchi nzima lenye lengo la kusaidia kuwawezesha wafanyabiashara na walipakodi wote nchini kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao ili waweze kuongeza uhiari wao katika kulipa kodi.
Mwenda ameongeza kuwa ufanisi huo wa makusanyo umetokana pia na muitikio mzuri wa wafanyabiashara wanaofanya biashara za mtandaoni kwa kampeni za usajili na ulipaji kodi zilizofanywa na TRA hasa kwa wale wanaofanya biashara za huduma ya malazi.
“Pia ufanisi huu umetokana na TRA kuendelea kusimamia utendaji kazi mzuri, kusimamia kwa ukaribu nidhamu na kuchochea ubunifu kazini kwa watumishi wote wa Mamlaka ya Mapato.
“Aidha kuendelea kuweka kipaumbele kuhakikisha watumishi wote wa TRA wanazingatia weledi katika utendaji kazi wao ikiwemo kuwapatia mafunzo ya kina watumishi wote wapya walioajiriwa kabla ya kuwapangia vituo vyao vya kazi imesaidia pia ufanisi huu,” amesema Mwenda.
Aidha Mwenda amesema kuimarisha usimamizi wa vyanzo vyote vya Forodha kupitia matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa, pamoja na kuboresha ufanisi katika uondoshaji wa mizigo katika vituo vyote vya Forodha umesaidia sana kupatikana kwa ufanisi huo.

