NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UMOJA wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama ( NSSC) umetoa Rai Kwa vyama vya siasa nchini kutokutumia wanafunzi katika kampeni za uchaguzi mkuu, ukisisitiza kuwa ni ukiukwaji wa haki za watoto na kinyume cha sheria.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Oktoba 1, 2025, jijini Dar es Salaam, wanachama wa umoja huo wamesema Kuna matukio ya baadhi ya shule wanafunzi kutolewa darasani ili kushiriki mikutano ya kampeni ni hatari kwa usalama, ustawi na haki ya mtoto ya kupata elimu.

Amina Ali, Mratibu wa Programu kutoka shirika la My Legacy amesema kuwa kuna viashiria vya ongezeko la matumizi ya watoto kwenye siasa, jambo linaloashiria kutoweka kwa mipaka ya kisheria kuhusu ushiriki wa watoto katika shughuli za uchaguzi.

“Tunahimiza vyama vyote vya siasa na wagombea kujitenga kabisa na matumizi ya watoto katika kampeni hili ni jambo linalohatarisha makuzi yao, linakiuka sheria, na linapaswa kuepukwa kwa gharama yoyote,” amesema Ali

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (Tanzania Bara) na Sheria ya Mtoto Zanzibar Na. 6 ya mwaka 2011, mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18, na haruhusiwi kushiriki katika shughuli za uchaguzi kwa namna yoyote iwe kwa kupiga kura, kugombea au hata kuhudhuria mikutano ya kampeni.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi kutoka taasisi ya HakiElimu Makumba Mwemezi amesisitiza kuwa jukumu la kuwalinda na kuwatetea watoto halipaswi kuishia katika matukio maalum kama uchaguzi, bali ni wajibu wa kudumu unaopaswa kutekelezwa na kila mmoja bila kujali hali ya kisiasa iliyopo.
“Tamko hili lilisomwa na dada Amina kwa niaba ya taasisi, linatoa wito kwa kila kundi kutambua na kutekeleza wajibu wake katika kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa, kutetewa na kuwekewa mazingira salama wakati huu wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kumalizika”amesema Mwemezi
Naye Meneja mradi kutoka Tanzania Child Rights Forum (TCRF),Rogasian Massawe ameeleza kuwa mazingira ya kampeni mara nyingi si rafiki kwa watoto kutokana na kelele, msongamano, lugha kali na wakati mwingine vurugu zinazoweza kutokea hivyo watoto Wala wanafunzi hawatakiwi kuwepo katika mazingira hayo
Cleopatra Ngesi ni Ofisa wa masuala ya watoto na vijana kutoka TAMWA ametoa rai kwa vyombo vya habari kuhakikisha kuwa havitumii picha au kauli zinazodhalilisha watoto katika taarifa zao za uchaguzi.
Amesema ni wajibu wa wanahabari kuwalinda watoto badala ya kuwafanya nyenzo za kisiasa.
Aidha mratibu wa mradi wa jukwaa la utu wa toto (CDF)Irene Ernest kutoka ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto hawaingii maeneo ya kampeni, vituo vya kupigia kura au mikusanyiko ya kisiasa kwa sababu si salama kwao.
“Wazazi wanapaswa kuwa walinzi wa mstari wa mbele wa watoto wao. Huu si wakati wa kuwaacha watoto mitaani au kuwapeleka kwenye mikutano ya kisiasa. Haki ya mtoto ya kulindwa ni ya kikatiba,” amesema Ernest

