NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM

MKUU wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kuwa jumla ya wanajeshi 125 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanatarajiwa kwenda nchini Lebanon kwa ajili ya ulinzi wa amani katika nchi hiyo.

Brigedia Jenerali Itang’are ameyasema hayo leo Septemba 17,2025 jijini Dar es Salaam wakati akiwaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa wanajeshi hayo wanaotarajiwa kwenda kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa (UN) katika nchi hiyo ya Lebanon.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuwaaga wanajeshi hao, Brigedia Jenerali Itang’are amesema tangu Aprili mwaka huu kundi hilo lilikuwepo chuoni hapo TPTC na kwamba wameshakamilisha mafunzo na wapo tayari kwa ajili ya kwenda kulinda amani katika nchi hiyo.
Amesema wanajeshi hao 125 watakuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kulinda amani kwa muda wa mwaka mmoja na kwamba Mkuu wa Majeshi nchini anawasisitiza waishi viapo vyao ili wanapokwenda huku waweze kuipeperusha vyema bendera ya Taifa.

“Kikundi hiki cha Polisi Jeshi tangu kilipopelekwa mwaka 2007, Umoja wa Mataifa (UN) umekuwa na imani kubwa na utekelezwaji wa majukumu yake na ndio sababu ya kuongeza ushiriki wa Tanzania katika kulinda amani kwenye maeneo mengine.

“Wanajeshi wetu wameweka historia kwani wameendelea kufanyakazi kwa uaminifu mkubwa na kwa Bahati nzuri hakuna tukio lolote la uvunjifu wa nidhamu tangu kuanzishwa kwake,” amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Kombani ya Polisi Jeshi kundi la 33/34-2025,Luteni Kanali Abdallah Hussein Rajab alisema kulingana na maelekezo waliyopewa na Makao Makuu ya Jeshi wamejipanga kwenda kutekeleza majukumu ya umoja wa mataifa kulingana na azimio walioanzisha misheni ya Lebanon toka mwaka 1978.
”Sisi tumejipanga kwanza kwenda kutekeleza maagizo au amri tuliyopewa na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania pia kutekeleza maazimio ya umoja wa mataifa kupitia operesheni wanayoenda kufanyia kazi,”amesema.
Kapteni Fatuma Adam Miongoni mwa wanajeshi wanaoenda nchini Lebanon Kulinda Amani amesema wao kama wanawake walichojipanga nacho ni kwenda kutekeleza majukumu yote ambayo yameainishwa na Jeshi pamoja na majukumu yote yaliyoainishwa na Umoja wa Mataifa.
”Tutakachokifanya huko ni kushirikiana na wenzao na kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwepo na kuwasaidia wanawake wanapokuwa katika majukumu yao.
”Changamoto zipo hususan kwa waathirika wa vita lakini tutajitahidi kupambana nazo kuziweka sawa,”amesisitiza.

