NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA kutoka Falme za Kiarabu, Oman, wamewasili nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na wawekezaji wa Kitanzania. Ujumbe huo, ukiongozwa na Dk. Salem Al-Junaibi – Mjumbe wa Baraza la Serikali na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya Mkoa wa Al Wusta – umepokelewa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA),Oscar Kissanga.
Aidha, ujumbe huo pia umepokelewa na Balozi Abdallah Kilima, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za Kiarabu, hususan Oman.
Katika mazungumzo yao, pande zote mbili zimeeleza dhamira ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kuongeza uwekezaji, na kubadilishana maarifa kati ya sekta binafsi za Tanzania na Oman.
Ziara hiyo inalenga kufungua milango kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kufikia masoko ya Kiarabu, sambamba na kuvutia wawekezaji kutoka Oman kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, na utalii.