NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHILINGI Milioni 100 /-zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB msimu wa sita kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo Jumapili Agosti 17,2025 katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson ameema mbio hizo zimeyaunganisha mataifa 27 na kuwakutanisha washiriki zaidi ya elfu 16 ambao kwa kukimbia kwao wameweza kuchangia matibabu ya watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo.


Dk.Tulia amesema CRDB Benki imeweza kusambaza tabasamu kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuhakikisha watoto zaidi ya 500 wenye magonjwa ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na afya zao kurejea.

Aidha Dk.Tulia aliwashukuru wadau wa Benki ya CRDB kwa kuungana na benki hiyo kukusanya fedha kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, wanawake wenye ujauzito hatarishi na vijana wanaohitaji kuinuliwa kiuchumi.
“Mchango unaotolewa na Benki ya CRDB katika sekta ya afya umemuwezesha Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kupata tuzo inayotambua kasi kubwa iliyopo katika kuboresha miundombinu ya afya, huduma za afya ikiwemo kushusha vifo vya mama na mtoto ambayo imemuweka kwenye historia duniani”, amesema Dk.Tulia.
Dk.Tulia alitoa wito kwa jamii kufanya mazoezi ili iweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuzingatia afya ya mwili kulisaidia taifa kuwa na watu wenye afya bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji kutoka Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema mbio za CRDB msimu wa sita zinaenda sambamba na kusherehekea miaka 30 ya benki hiyo huku akiainisha kuwa kwa kipindi chote hicho benki hiyo imekuwa ikichukua asilimia moja ya pato lake na kurudisha katika jamii kupitia michezo, afya, elimu na mambo mengine.
“Katika mbio hizi za msimu wa sita tulijiwekea malengo ya kupata Bilioni 2 ambazo kwa hakika tumeweza kuzipata na hivyo tumeelekeza kiasi cha Tshs. Milioni 100 katika Hospitali ya CCBRT kusaidia wanawake wenye ujauzito hatarishi, Milioni 100 kwenda JKCI kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo na Milioni 250 kwaajili ya programu mbalimbali za vijana”, amesema Nsekela
Nsekela amesema misimu sita ya mbio za CRDB imekuwa ikiwawezesha wadau wake wakuu watatu wakiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya CCBRT na Vijana kupitia programu mbalimbali za maendeleo.
–

