NA MWANDISHI WETU,MANYARA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara imemtia hatiani Mtendaji wa Kata ya Kainam,Eliwangu Mkumbwa kwa kosa la ufujaji na ubadhirifu wa fedha za mradi wa Kituo cha Afya Kainam .
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa Mkumbwa alizitumia fedha hizo kwa manufaa yake binafsi.
Aidha katika shauri la uhujumu uchumi Namba 13987/2025,Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 28(1) sura ya 329 cha mwaka 2023 vikisomwa pamoja na aya ya 21 katika jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga Sura ya 200 ya mwaka 2023.
Kesi hiyo imeendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU) Neema Gembe.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi Wilaya ya Mbulu Vitus Kapugi alisema Mahakama amemtia hatiani mshtakiwa baada ya kufanya makubaliano (plea bargaining agreement) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mshtakiwa amepewa adhabu ya kulipa faini ya kiasi cha Sh. 100,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani iwapo atashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha pamoja na kurejesha fedha alizozifanyia ubadhirifu kiasi cha Sh. 3,129,000/- kwa Muathirika
Hadi hukumu inasomwa mshtakiwa alikuwa amefanikiwa kurejesha kiasi cha Sh. 1,560,000/- katika akaunti ya Kainam Community Account iliyopo Benki ya NMB na kiasi kilichobaki atatakiwa kurejesha kabla au ndani ya miezi sita kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba wa makubaliano ( plea bargaining.)