▪️Ni hatua ya kuiimarisha STAMICO kiuchumi
▪️Aelekeza Wachimbaji wadogo kupewa leseni za uchimbaji na kurasimishwa
▪️Waziri Mavunde awataka STAMICO kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18
▪️Wachimbaji wadogo wamshukuru Rais Samia kwa kuwajali
NA MWANDISHI WETU, LINDI
WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde (Mb) amebainisha kuwa Dk Samia Suluhu Hassan ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kutolewa kwa leseni ya uchimbaji madini ya nikeli kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kwa Wachimbaji wadogo waliokuwepo katika eneo la vilima vya Ntaka- Nachingwea,mkoani Lindi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Julai 08, 2025 katika mkutano wa hadhara wa wananchi na wachimbaji katika Kijiji cha Nditi punde tu baada ya kufanya ziara ya kutembelea maeneo na migodi ya wachimbaji wadogo chini ya Umoja wa Vikundi vya Wachimbaji Madini (UVIWAMA).
” Rais Dk.Samia S. Hassan amesikia kilio chenu cha muda mrefu cha kutaka kupewa maeneo ya uchimbaji katika Leseni inayomilikiwa na Serikali. Na ndiyo maana nimefika hapa kuja kuwaletea habari njema wachimbaji wadogo kwamba, hatutawaondoa katika eneo mnalochimba na tunakwenda kuwarasimisha.”
Pamoja na kupewa eneo la uchimbaji, naomba niwasihi wachimbaji wadogo kufuata taratibu kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123 ambayo inaelekeza mwenye haki madini kuhakikisha anapata ridhaa ya mwenye haki ardhi kabla hajaanza uchimbaji, ili kuepusha migogoro katika shughuli zao za uchimbaji.
Rais Dk. Samia ameelekeza eneo la leseni hiyo lenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 45 ipewe Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa ajili ya kuanza uchimbaji mkubwa wa nikeli ndani ya miezi 18 ijayo kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
Kwakuwa kwenye Leseni hii serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 243 kama fidia, ni lazima sasa STAMICO na wachimbaji wadogo wafanye uchimbaji wenye tija ili kurejesha fedha hizo katika mfuko mkuu wa Serikali”Alisema Mavunde
Awali, akitoa salam kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Lindi (LIREMA), Mayunga Musa Buyaga amesema wachimbaji wadogo wanamshukuru sana Rais Dk.Samia Hassan kwa upendo mkubwa na kuwajali na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kufanya uchimbaji wenye tija.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amempongeza Rais Dk.Samia kwa kurudisha matumaini na nyuso za furaha kwa wachimbaji wadogo na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili shughuli za uchimbaji zifanyike kwa utaratibu uliowekwa pasipo kuzalisha migogoro.