NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) limetoa wito kwa wananchi wanaokwenda katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) kutembelea banda lao ili kupata elimu zaidi kuhusu masuala ya Bima.
Ofisa Uhusiano wa NIC, Ephrasia Mawala, amebainisha hayo leo Jumapili Julai 6, 2025 wakati akizungumza na Demokrasia katika maonesho hayo yanaendelea jijini Dar es Salaam.
“Mwitikio wa wananchi kuja katika banda letu ni mkubwa na wanakuja kupata elimu kuhusu bima na baadhi yao tayari wanabima na wanakuja kufuatilia hatua zilizofikia katika madai yao kutokana na changamoto ambazo wamepata hususan kwenye vyombo vyao vya usafiri.
“Kwa kifupi naweza kusema kwamba huduma zote zinazohusiana na upatikanaji wa bima zinaendelea kutolewa hapa hapa Sabasaba kwenye banda letu hivyo wananchi wafike tutawapa huduma stahiki,” amesema.
Ameongeza kuwa kama ilivyokawaida pindi wanaposhiriki maonesho hayo wanatoa elimu kuhusu bima kwaajili ya kuwajengea uelewa wananchi ili waone umuhimu wake katika maisha.
Amefafanua kuwa wanatoa Bima ya Maisha ambayo inatoa dhamana ya kifedha kwa wahusika au wategemezi wa mteja endapo mteja huyo atakuwa amekumbwa na janga la kifo.
Pia amesema wanatoa bima nyinginezo ikiwemo ya ajali, bima ya mali na kilimo, hivyo amewasisitiza wananchu mbalimbali wanaofika katika maonesho hayo kufika banda la NIC kupata elimu kuhusu masuala ya bima.