*AWASHAURI WANAOKWENDA SABASABA KUFIKA BANDA LA WIZARA YA FEDHA
*LENGO NI KUPEWA ELIMU SAHIHI JUU YA KODI
NA WAANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WANANCHI wametakiwa kuwa na uelewa kuhusu Sera za Kodi zinazoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa lengo la kumfanya mwananchi kulipa kodi kwa hiari ili kuisaidia Serikali kutoa huduma bora na endelevu katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, maji, barabara, nishati na kilimo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,Jenifa Omolo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na mabanda mengine kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) ambayo yameanza Juni 28 na kutarajiwa kuhitimishwa Julai 13 mwaka huu.
Alisema kuwa Bunge limepitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Kiasi cha Sh. Trilioni 56.49 ambayo inalenga pamoja na mambo mengine kutekeleza miradi yenye faida ya moja kwa moja kwa mwananchi kama barabara, nishati, maji na kilimo.
Omolo alisema kuwa jukumu la mwananchi katika kufanikisha hilo ni pamoja na kulipa kodi kwa hiari kwa mazingira rafiki ambayo yanatokana na Sera nzuri za kodi ambazo zimeandaliwa na Wizara ya Fedha.
Ametoa rai kwa wananchi wanaotembelea katika Maonesho hayo kufika Banda la Wizara ya Fedha ili kukutana na wataalamu ambao watawapa elimu ya Sera ya Kodi na faida zake kwa jamii.
Omolo amewahakikishia wananchi kupata huduma bora kutoka Serikalini kupitia Bajeti iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa gharama nafuu.
Aidha, alisema kuwa ndani ya Banda la Wizara ya Fedha inatolewa elimu ya huduma ndogo za fedha kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha ili kuondokana na kuchukua mikopo isiyo na tija.
Alisema pia kuwa Banda la Wizara ya Fedha linashirikisha Vyuo vikuu vilivyo chini ya Wizara ambavyo vinatoa elimu kuhusu kozi mbalimbali ambapo alivitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Aidha alisema kuwa wataalamu wengine ni kutoka Idara na Vitengo vya Wizara hiyo na Taasisi zake ikiwa ni pamoja na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Mfuko wa Dhamana na Uwekezaji Tanzania (UTT AMIS), Mfuko wa Self Microfinance, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Taasisi nyingine ni pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), Benki ya Maendeleo TIB na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Hazina SACCOS, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).