NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WADAU wa zao la mkonge wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta ya Mkonge na kujifunza uongezaji thamani wa zao hilo katika matumizi mbalimbali.
Wito huu umetolewa na
Mkuu wa Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), David Maghali alipokuwa akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika katika banda la Bodi hiyo kujifunza kuhusu Kilimo bora cha Mkonge na faida zake na Sekta ya Mkonge kwa ujumla katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Mkonge ndiyo zao la biashara pekee lenye matumizi mengi, linaweza kutumika katika kutengeneza bidhaa kama vile mazulia, magunia, mabegi na vikapu
“Pia mkonge unaweza kutumika katika ujenzi, uundaji magari na mabaki ya Mkonge yanaweza kuzalisha protini inayotumika kwenye chakula cha mifugo. Haya ni baadhi tu ya matumizi kati ya mengi yaliyopo,” amesema Maghali.
Pamoja na mambo yote Bodi ya Mkonge imetumia nafasi hiyo kuwakaribisha wadau na wananchi kutembelea katika banda lake lililopo katika Ukumbi wa Katavi (Katavi Hall) kwenye Banda la Wizara ya Kilimo.