NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara za huduma za kifedha ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwa kuwa maendeleo endelevu ya taifa hayawezi kufikiwa bila ushiriki thabiti wa sekta binafsi.
Amesema kuwa sekta ya fedha ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa Uchumi na ustawi wa wananchi kwa ujumla na ni moja ya sababu inyowezesha maendeleo ya Taifa kwenda kwa kasi.
Amesema hayo leo Alhamisi (Julai 03, 2025) wakati wa uzinduzi wa Benki ya Maendeleo PLC, kuwa Benki kamili ya kibiashara, kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
“Endeleeni kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu, serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha katika kuchagiza maendeleo, imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia bunifu”.
Katika hatua nyingine,Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha zikiwemo benki kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kuelewa, kutumia na kunufaika na huduma za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Tukifanya haya tutapunguza wizi, upotevu wa fedha kiholela kwa sababu kila mmoja atakuwa anaweza kujua fedha yake ataipataje, ataihifadhi wapi na namna ya kutoa lakini pia wapeni wateja wenu namna ya utunzaji wa fedha”
Pia,Majaliwa ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Finscope huduma jumuishi za fedha zimeweza kukua kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2023.
“kwa mujibu wa utafiti huo, matumizi ya huduma za benki yameongezeka na kufikia asilimia 22 mwaka 2023 kutoka asilimia 17 mwaka 2017”.
Kadhalika, Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za fedha zijenge mifumo rahisi na rafiki kwa makundi yote ya watumiaji wa huduma za kifedha.
Awali, Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa, Mwakilishi wa Askofu Dean Chadiel Lwiza ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuisimamia benki hiyo na kuwa mfano wa benki iliyoanzishwa na wazawa kwa mtaji mdogo hadi kufikia kuwa benki kitaifa. “Tunaiomba benki kuu jicho lenu liwe kali kuliko letu, itazameni hii benki”
Kadhalika, ameongeza kuwa sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji katika biashara na usimamizi mzuri za biashara. “Tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoomgizwa na Rais Dk. Samia kwa kuendelea kuweka mazingira haya mazuri ya ufanyaji biashara”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau amesema kuwa benki hiyo imejiweka katika nafasi bora zaidi ya kuwa benki ya kisasa, shindani na jumuishi kwa Watanzania wote hasa kipindi dunia inapoelekea kwenye zama mpya zenye msukumo wa kiteknolojia, ubunifu, na uwajibikaji wa hali ya juu.
“Kwa kufanya hivyo, tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dk.Samia Suluhu Hassani, yenye dhamira ya kuwafikia watanzania wengi zaidi nchi nzima kupitia dira ya taifa ya ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion) na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta binafsi, tutaendelea kushirikiana na Serikali, katika ujenzi wa Uchumi wa nchi”.
Naye, Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande ameipongeza benki hiyo kwa hatua kuwa iliyofikiwa na benki hiyo katika utoaji huduma kwa watanzania hasa kwa kutumia fursa zilizowekwa na Serikali “Sisi Wizara ya Fedha tumeendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki ya ufanyaji wa shughuli za kifedha, sasa wekeni mkakati wa kuifikisha benki hii maeneo mengi zaidi”.