NA ANDREA NGOBOLE, ARUSHA
WATAALAMU wa uhifadhi nchini, wametakiwa kubuni Teknolojia rahisi zitakazopunguza migogoro baina ya binadamu na Tembo.
Serikali hutumia takriban sh 4 bilioni kila mwaka, kulipa fidia kwa wananchi wanaodhurika na tembo na wanyamapori wengine nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI), Dk. Ernest Mjingo akizindua mradi wa kukabiliana na migogoro baina ya Tembo na Binadamu katika eneo la Ikolojia ya Tarangire -Manyara, alisema changamoto ya Tembo imekuwa ni kubwa katika maeneo mengi nchini.
Dk. Mjingo alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo ni muhimu kuendelea kubuniwa teknolojia ambazo ni rafiki kwa wananchi ili zitumike kudhibiti tembo kuendelea kuvamia mazao na kufanya uharibifu.
Alisema kila siku wahifadhi na watafiti, wanapaswa kubuni mbinu mpya za kukabiliana na Tembo, kwani Tembo nao wana akili ambazo zinawafanya kubadilisha mbinu zao za kufanya uvamizi.
Dk. Mjingo alisema mbinu hizo, zinapaswa ziende kwenye jamii ili jamii izielewe vizuri na kuweza kuzitumia kwa muda mrefu kukabiliana na migogoro baina ya Tembo na Binadamu.
Hata hivyo, alisema kuongezeka kwa Tembo nchini ni mafanikio ya kuimarishwa uhifadhi na sasa kinachopaswa kufanywa ni kuendelea kuwa na uhifadhi endelevu lakini pia wananchi wananufaika kiuchumi.
Dk. Mjingo alipongeza shirika lisilo la kiserikali la uhifadhi la Tembopilipili kuja na mradi wa kudhibiti tembo kupitia ufugaji wa nyuki, mradi ambao utafanyika katika vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Tembo pilipili, Dk.Alex Chang’a alisema taasisi hiyo tangu mwaka 2009 imekuwa na miradi ya kupunguza migogoro baina ya Tembo na binaadamu maeneo mbali mbali nchini.
Dk. Chang’a alisema katika mradi huo mpya uliozinduliwa unafadhiliwa na taasisi ya Vetenary without border ya Sweden kwa zaidi ya Sh.Milioni 50 na unatarajiwa kutekelezwa katika Kijiji cha Kakoi wilayani Babati.
“Katika utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza tunafunga uzio wa mizinga 100 ili kuzuia Tembo kuvamia makazi na mashamba lakini pia kutazalishwa asali kwa wananchi na hivyo kuwa moja ya faida za kiuchumi”alisema
Alisema katika utekelezwa wa mradi huo, malengo ya jumla ni kuwa na mizinga takriban 500 katika vijiji ambavyo vitahusika katika mradi huo, ambao ni sehemu ya mradi wa muda mrefu katika eneo hilo kupunguza migogoro baina ya binaadamu na wanyamapori.
“Leo tumekutana hapa tutowe Mawazo, tuna watafiti wa wanyamapori, wataalam wa ufugaji nyuki, watafiti na wasomi Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Wanahabari wa masuala ya uhifadhi na watendaji wa serikali katika sekta ya uhifadhi na Utalii”alisema
Dk. Chang’a alisema katika usimamizi wa mradi huo, kutakuwa na maafisa katika vijiji ambavyo vitatekeleza mradi ili kuwepo na usimamizi wa kila siku lakini pia umiliki wa mradi utakuwa wa ubia baina ya wananchi na Tembopilipili ili kuwepo na uendelevu wa mradi huo.
“Tunakusudia kuwa na Kituo cha Utalii, ambapo asali na mazao mengine ya Nyuki yatauzwa kwa watalii wanaofika Tarangire na wananchi wengine”alisema.
Akitoa mada katika ufunguzi huo, Msimamizi wa mradi wa Tembo Tarangire Revocatus Meney na mtafiti wa miradi ya ufugaji nyuki wa TAWIRI, Dk. Wilfred Marealle kwa Pamoja walieleza mradi huo ni mzuri na utapunguza migogoro baina ya Tembo na binadamu.
Meney alisema TAWIRI wameendelea na utafiti wa Tembo katika eneo la Tarangire na kubaini idadi ya Tembo inaendelea kuongezeka na sasa wameainisha makundi 19 ya tembo takriban 4000 waliopo Tarangire.
Hata hivyo, alisema manufaa ya mradi huo, yataonekana kukiwepo na usimamizi mzuri, utunzwaji wa kumbukumbu na ushirikishwaji wa jamii ili kuona faida za ufugaji nyuki lakini pia kupunguza madhara ya Tembo.
Dk.Marealle alisema TAWIRI imeimarisha kitengo cha ufugaji nyuki kwa kutoa ushauri za kitaalam ili kuwezesha wananchi kufuga nyuki kwa kuzuia Tembo kuvamia mashamba na makazi yao.
Katika uzinduzi huo, wataalam wa uhifadhi na watafiti, walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali ili kuboresha mradi huo kwa manufaa ya uhifadhi na wananchi kwa ujumla.