*AIPONGEZA TET KWA UTEKELEZAJI MZURI WA MAJUKUMU YAKE
*DK.KOMBA AISHUKURU BENKI YA DUNIA
*WALIMU WAJINYAKULIA VITITA VYA FEDHA
NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Carolyne Nombo kupanga bajeti ya kuendesha Tuzo za Stadi za Kufundishia na Ujifunzaji kwa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari ili ziwe za kudumu.
Maelekezo hayo ameyatoa jana Jumamosi Jioni Julai 14, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizo kwa msimu wa tatu zenye lengo la kuchochea walimu kuwa wabunifu kwa kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji.
“Hili jambo la kutoa tuzo ni zuri na linafanyika kwa kuwa linadhaminiwa na Benki ya Dunia (WB), hivyo nasi tuanze kuandaa bajeti ili ziwe za kudumu, sasa Katibu Mkuu katika vikao vyenu hakikisheni mnaandaa bajeti ya tuzo hizi, ingawa (WB) bado tunawahitaji,” amesema.
Pia aliwakumbusha walimu, kuzingatia kauli ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassani, aliyoitoa Feb 1, mwaka huu jijini Dodoma wakati akizundua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 ambapo alisema “Katika michakato yote inayofanyika walimu hatutawasahau hususan katika maslahi yao”.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa ndio maana wanatoa tuzo hizo kwa kuwa wanathamini mchango wa walimu kutokana na kazi kubwa wanayoifanya kufunza vijana, kuwalea na kuwajenga katika misingi bora.
Aidha aliipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kusimama imara katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo katika usimamizi na uendelezaji wa tuzo hizo na kuziboresha ambapo zimefanyika kwa msimu wa tatu mfululizo.
“Wakati tunaanza tulianza na Walimu wa Shule za Msingi, lakini nashukuru mkajiongeza na sasa mmeongeza na wa Sekondari hayo ni mafanikio makubwa na ninawapongeza kwani hamjawahi kutuangusha,” amesema.
Dk. Charles Mahela, Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu ya Msingi katika wizara hiyo , akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Nombo, amesema tuzo hizo zinafanyika kutokana na maelekezo yake Waziri Prof Mkenda, hivyo maagizo mengine yataendelea kutekelezwa ili kuleta tija katika nyanja mbalimbali ya elimu.
Naye Mkurugenzi wa TET, Dk. Aneth Komba amesema tuzo hizo zinatoa fursa kwa walimu kuonesha umahiri wao wa kufundisha kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwani inamsaidia mwanafunzi kufanya vizuri katika maisha baada ya kuhitimu masomo yake.
Ameongeza kuwa shindano hilo lina lengo la kutoa fursa kwa walimu wa somo la Sayansi, Shule za Msingi na Hisabati na Sayansi kwa kidato cha kwanza kuonesha umahiri wao wa kutumia Tehama na mbinu shirikishi katika ufundishaji ili kuleta chachu katika kukuza Stadi ya Karne ya 21.
Ameongeza kuwa katika kuwapata washindi, walimu walituma video zao walizojirekodi wakiwa wanafundisha na zilichujwa kuanzia ngazi za Halmashauri hadi Taifa kupitia wataalamu wenye sifa na kufanikisha kupatikana washindi.
“Changamoto kubwa ambayo tumeipata ni baadhi ya walimu kurekodi maudhui ambayo yapo nje ya makusudio, tunawaomba katika msimu ujao wazingatie kinachohitajika na washiriki,” amesema.
Pia aliishukuru WB Kwa kuendelea kudhamini shindano hilo kupitia miradi ya Boost na Sequip inayokusudia kuongeza uwezo WA walimu katika nyanja ya ufundishaji na ujifunzaji kupitia mafunzo endelevu Kwa walimu kazini (MEWAKA).
Kwa upande wake, Gema Toddy ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete amesema wanafadhili miradi mbalimbali ya elimu hapa nchini na kufafanua kuwa ili kuwa na elimu bora ni lazima mwalimu awe bora na ndio sababu iliyowasukuma kufadhili tuzo hizo.
“Wakati tunaanza kudhamini tuzo hizi, tulianza na Walimu wa Shule za Msingi na sasa tumeongeza wigo hadi Sekondari, lengo letu ni kuhakikisha kunakuwa na walimu bora watakasaidia kuwa na elimu bora na kutengeneza wanafunzi bora,” amesema.
Katika hafla hiyo, mshindi namba 10 hadi 4 kwa masomo ya Fizikia, Kemia, Hisabati, Biolojia na Sayansi walipatiwa vyeti na washindi wa tatu walijinyakulia kitita cha Sh.Milioni 2.5, wa pili Milioni 3/- na washindi wa kwanza walijizolea kitita cha Sh.Milioni 4/-
Walimu wa shule za msingi waliojinyakulia nafasi ya tatu katika shindano hilo kwa msimu huu ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Ntandi, Haji Mohamed, Mwalimu Theresia Rogath wa Shule ya Msingi Sombetini Arusha na Mwalimu Teleza Boniphace wa Shule ya Msingi Mahina Mwanza.
Walioshika nafasi ya tatu kwa upande wa Sekondari ni Halfani Hamisi wa Chidy Sec iliyopo Masasi mkoani Mtwara (Fizikia), Kleruu Sumaye wa Shule ya Sekondari Mringa iliyopo mkoani Arusha (Kemia), Hongera Nguvile wa Shule ya Sekondari ya wasichana Buseke(Hisabati) na Zakaria Bujingwa wa Shule ya Sekondari Mkata Handeni Tanga.
Walioshika nafasi ya pili ni Jema Mkonongo wa Sekondari ya Tandale (Dar es salaam), Neema Diliwa wa Sekondari ya Makumbusho (Kinondoni Dar es salaam), Emmanuel Mkama wa Melela Sekondari (Morogoro) na Athur Simkonde.
Walioshika nafasi ya kwanza ni King Kigongo wa shule ya Msingi Nassoro Seif (Morogoro), John Patrick wa Sekondari ya Muungano ya Usariver Arusha, Peter Lymo wa Sekondari ya Kilangale (Same Kilimanjaro) na Samuel Adriano wa Sekondari ya Madibira ya Mbeya.