NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo ametangaza vipaumbele vitano vya mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Prof. Mkumbo ametaja vipaumbele hivyo wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na mpango huo wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma leo Alhamisi Juni 12, 2025.
Prof. Mkumbo amesema kipaombele cha kwanza ni Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi na kwamba eneo hilo litajikita katika kutekeleza miradi na programu za maendeleo zinazolenga kuongeza uwezo wa nchi kikanda na kimataifa; kuimarisha utulivu na uendelevu wa viashiria vya uchumi jumla; kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara; na kuendeleza miundombinu ya usafiri na usafirishaji, Tehama na nishati.
Amesema kipaumbele cha pili ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma na kwamba eneo hilo litajielekeza katika programu na miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uzalishaji viwandani.
Mkumbo amesema eneo la tatu ni
kukuza uwekezaji na biashara, Programu na miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo itajielekeza katika kuimarisha mifumo ya kitaasisi, sera na sheria za kodi ili kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji.
Eneo la nne ni kuchochea maendeleo ya watu: Programu na miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika eneo hili itajielekeza katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji, mifumo na miundombinu ya elimu, afya, maji na mazingira; kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati; kukuza ujuzi kwa vijana, na kutoa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu wa elimu ya juu.
“Eneo la tano ni kuendeleza rasilimali watu, hili linajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kujiajiri.
Vile vile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu ambavyo ni muhimu katika kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo,” amesema Prof. Mkumbo