NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa hadi Aprili 2025, deni la Serikali lilikuwa Sh. Trilioni 107.70 na kwamba kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh. Trilioni 72.94 na deni la ndani ni Sh.Trilioni 34.76.
Dk. Mwigulu ameyasema hayo leo Juni 12, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajetu Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema kuwa tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Oktoba 2024 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu na kwamba katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2024/25 thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55.
Pia amesema inaonesha kuwa thamani ya sasa ya deni la nje kwa pato la Taifa ni asilimia 23.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.
“Machi 2025, kampuni ya Moody’s Investors Service ilifanya zoezi la mapitio ya kwanza ya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa mwaka 2025. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, kampuni hiyo ilichapisha matokeo ambayo yameendelea kuiweka Tanzania katika daraja la B1 kama ilivyokuwa kwa matokeo ya mwisho ya mwaka 2024,” amesema Dk. Mwigulu na kuongeza
“Kampuni nyingine kubwa ya Fitch Ratings inaendelea na mapitio ya kwanza kwa mwaka 2025 na inatarajia kuchapisha matokeo hivi karibuni. Kampuni hiyo ilichapisha matokeo ya mapitio ya mwisho Desemba 2024, ambapo iliiweka Tanzania katika daraja la B+,” amesema.
Dk. Mwigulu amesema matokeo ya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa yanaendelea kuipa taswira chanya nchi
katika medani za kimataifa na kwamba matokeo hayo ni bora kuliko nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na jitihada za Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kukuza uchumi,kusimamia kwa makini deni la Serikali na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha deni linaendelea kuwa himilivu ikiwemo: Kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo katika ugharamiaji wa bajeti; kuelekeza fedha za mikopo katika miradi inayokuza mapato ya ndani na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi; na kuendelea kuwahimiza maafisa masuuli kuzingatia maandalizi ya msingi ya miradi kabla ya kuingia mikataba kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuepuka ongezeko la gharama za mradi unaokopewa fedha.