NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeutaarifu umma wa Watanzania na kuwaalika wadau wa elimu na maendeleo, kwa ujumla kushiriki katika Maadhimisho ya kumi ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya UDSM yatakayofanyika kuanzia Juni 9- 11, 2025 katika Viwanja ya Maktaba ya Chuo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti, Prof. Nelson Boniface amesema kuwa Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 11, 2025 na mazungumzo ya mashirikiano ya kimkakati, kongamano, maonesho na mawasilisho ya watafiti na wabunifu likiwa ni jukwaa la washiriki kupata fursa ya kubadilishana maarifa na ushirikiano.
Aidha, Prof. Boniface amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Kutumia teknolojia ya Dijitali ili kukuza utafiti, ubunifu na ubiasharishaji,”.
Ameongeza kuwa miradi mingi itakayooneshwa ni ile ya wanafunzi na Wanataaluma huku akitanabaisha kuwa mtoa Mada Mkuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Peter Ulanga na Profesa Lilian Kaale Mkurugenzi katika masuala ya Ubunifu UDSM.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatumia fursa hiyo kujipambanua kwa jamii kwa kuonesha shughuli zake za utafiti, ubunifu, huduma kwa umma na ubadilishanaji maarifa kwa kuunga mkono DIra ya Taifa ya Maendeleo 2050.