NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
CHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) pamoja na Chemba ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC), zimetilina saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa pande tatu (Tripartite Agreement) na kampuni ya biashara kutoka Oman, business gateway International.
Lengo kuu la makubaliano hayo ni kuanzisha na kuimarisha mtandao wa pamoja wa masoko kati ya wafanyabiashara kutoka Tanzania Bara, Zanzibar, na Oman, ili kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande hizo tatu.
Hatua hii muhimu ya ushirikiano wa kibiashara inakuja ikiwa ni matokeo chanya ya ziara za kihistoria zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi nchini Oman.
Hafla ya utiaji saini imefanyika katika ofisi mpya za TCCIA zilizopo katika Jengo la PortView, Mtaa wa Gerezani, jijini Dar es Salaam.
Tukio la utiaji Saini limeshuhudiwa na viongozi wakuu wa taasisi husika, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Oscar Kissanga, Mkurugenzi Mtendaji wa ZNCC, Hamad Hamad, na Mkurugenzi wa Businessgateway International, Hafidh Al-Mahruqi.
Kupitia makubaliano haya, pande husika zimefungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kibiashara kati ya Oman na Tanzania, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kupitia biashara na uwekezaji wa kimataifa.