*Uongozi TCCIA wampongeza Samia
NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
UAMUZI uliotolewa na Serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo utaenda mbali sana katika kurahisisha uboreshaji wa vichocheo muhimu vya ukuaji kama vile nishati safi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kissanga, anasema kuanzishwa kwa benki hiyo kutachangia ongezeko la ufadhili katika sekta hiyo na pia kuongeza ukuaji na maendeeo ya sekta kwa ujumla.
“Kama tunavyofahamu, sekta yetu ya kilimo inahitaji msukumo wa ziada, hasa kwa kuwa inategemea kwa kiasi kikubwa wakulima wadogo wa kujikimu ambao ni wengi, hata hivyo wkullima hawa hukabiliwa na changamoto kubwa ya kupata mikopo kutoka benki za kibiashara zilizopo,” anasema Kissanga.
Anampongeza Rais Samia kwa uamuzi huo kwa sababu utawezesha pia biashara katika sekta ya kilimo ambayo bado ni uti wa mgongo wa uchumi kwani inaajiri watu wengi, huzalisha chakula cha kutosha kwa taifa, na pia huchangia katika kupata fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje.
Akizungumzia Mkutano wa Nishati Afrika 2025 uliofanyika Dar es Salaam, kiongozi huyo wa TCCIA anasema mkutano huo ulikuwa wa kihistoria katika taswira ya nishati ya bara la Afrika, ukivuta hisia kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Kwa kuzingatia malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu, Mpango wa Mission 300 unalenga kutekeleza suluhisho la nishati safi na mbadala kama vile nishati ya jua, upepo, na jotoardhi. Miradi hii ni muhimu sana katika kufanikisha malengo ya Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa,” anabainisha.
Kupitia mpango wa Rais Samia wa nishati safi, sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kutoa suluhisho la nishati ya gharama nafuu, mbadala, inayosaidia mazingira na pia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme barani Afrika.
“Tunajua kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo barani Afrika, hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba vipengele vyote vinavyochangia vinaangaliwa kwa njia ya kisasa kwa msaada wa fedha za uhakika na nafuu,” anasisitiza.
Katika mkutano huo wa AES 2025, Rais Samia aliahidi kuendelea kuwekeza katika miradi ya nishati safi ili kuiwezesha nchi kuachana na matumizi ya mafuta ya visukuku yanayolaumiwa kwa kuchochea mabadiliko ya tabianchi ambayo huathiri kilimo.
Katika hotuba yake kuu, Dk. Samia alieleza dhamira thabiti ya serikali yake ya kuhakikisha mazingira rafiki ya uwekezaji katika miradi ya nishati.
Alionesha hatua ambazo Tanzania imechukua katika kupanua miundombinu ya nishati, kuboresha ufanisi wa gridi ya taifa, na kukuza matumizi ya nishati safi.
“Tanzania imejizatiti kuunda mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa sekta binafsi katika nishati safi na ya kuaminika. Tunatambua kwamba nishati endelevu ni uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi, na tunakaribisha ushirikiano utakaowezesha ubunifu na kuongeza upatikanaji wa nishati nchini na barani Afrika,” alisema Rais huyo.
Kiongozi wa nchi alisisitiza nafasi ya Tanzania kama kiongozi wa kikanda katika sekta ya nishati, akitaja jitihada za kimkakati za nchi katika kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme na kuunganisha vyanzo vya nishati mbadala kwenye gridi ya taifa.
“Tanzania imejizatiti kupunguza utegemezi wa mafuta ya visukuku kwa kukuza miradi ya nishati ya maji, jua, na upepo, kwa kuendana na malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu,” alisisitiza Rais Samia huku akitoa ahadi ya kutatua changamoto za muda mrefu za sekta binafsi kuhusu ufadhili.
Mfumo wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za maendeleo umelenga kuunda mazingira bora kwa ajili ya uwekezaji wa sekta binafsi.
Alieleza kuwa Taasisi ya Rockefeller, Benki ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine wanafanya kazi na serikali za Afrika kushughulikia vikwazo vya kisheria na sera vinavyoweza kuzuia ushiriki wa sekta binafsi.
Kama sehemu ya mkakati mpana wa nishati wa Tanzania, mpango wa Mission 300 ni hatua ya kishujaa kuelekea kubadilisha mustakabali wa nishati barani Afrika.
Lengo kuu ni kuwapatia umeme watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni jitihada za kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa zaidi ya watu milioni 600 barani Afrika, ambapo takribani watu milioni 571 katika Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara hawana umeme.
Chemba hiyo ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele ajenda ya diplomasia ya uchumi ya Rais, hivi karibuni iliandaa mkutano wa majadiliano kati ya sekta binafsi na serikali kupitia Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, pamoja na ujumbe kutoka Shirikisho la Chemba za Biashara la Saudi Arabia, uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Februari.
Mkutano huo wa ngazi ya juu haukulenga tu kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Saudi Arabia, bali pia kuendeleza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
“Mkataba wa kihistoria ulisainiwa kati ya TCCIA na Shirikisho la Chemba za Saudi Arabia mbele ya Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji,” anabainisha Kiongozi huyo wa TCCIA