NA MWANDISHI WETU,SINGIDA
WADAU wa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Singida wameithibitishia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi juu ya nia yao ya kutaka kubadili jina la Jimbo la Singida Kaskazini kuwa Jimbo la Ilongelo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ameongoza timu ya Tume iliyotembelea Singida na kufanya kikao kati ya Tume na Wadau wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.
Kikao hicho cha siku moja kililenga kuthibitisha kuwa maombi yaliyowasilishwa ya mapendekezo ya kubadili jina la Jimbo la Singida Kaskazini, Halmashauri ya Wilaya ya Singida Mkoa wa Singida ni sahihi kwa mujibu wa barua iliyowasilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa.
“Tulipokea maombi ya mapendekezo ya kubadili jina la jimbo la uchaguzi la Singida Kaskazini kupitia barua yenye Kumb. Na. CAB.95/226/02C/140 ya tarehe 28 Februari, 2025 kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida,” alisema Jaji Mwambegele.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga aliithibitishia Tume juu ya barua hiyo na kusema ni kweli ofisi yake.
Naye Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo aliithibitishia Tume kwa niaba ya Madiwani wa Halmashauri ya Singida Vijijini kuwa walihitaji mabadiliko hayo yaendane na jina la eneo lao.
Jaji Mwambegele aliwaambia kuwa baada ya kufanyika kwa kikao hiko, haina maana kwamba ombi lao limekubaliwa, bali Tume imetimiza matakwa ya kanuni ya 18 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024 za kutembelea majimbo yaliyoomba kugawanywa au kubadili jina.
“Hivyo, Tume itakutana na kuendelea kuchakata taarifa zote na baada ya hapo kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria, itatangaza majimbo yaliyogawanywa na au kubadilisha majina,”alisema Jaji Mwambegele.