NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema kuwa sababu za ubadhirifu kuendelea kujitokeza kwenye ukusanyaji wa mapato ya halmashauri mbalimbali nchini ni baadhi ya wasimamizi na wahasibu kushirikiana na wakusanyaji kujinufaisha na fedha hizo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 27, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila wakati akiwasilisha ripoti ya utendaji wa taasisi hiyo ya mwaka 2023/2024 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaa.
Chalamila amesema sababu nyingine ni kukosekana kwa usimamizi Madhubuti katika kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinapelekwa benki na baadhi ya wasimamizi kukosa uadilifu.
“Hivyo ni vema viongozi wa Halmashauri wakaimarisha usimamizi kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato ya serikali,” amesema Chalamila
Aidha Chalamila amesema kuwa wamekamilisha uchunguzi wa majalada 728 na kuwezesha kuchukua hatua mbalimbali kwa mujibu wa sheria, ambapo kati ya majalada hayo 17 ni ya rushwa kubwa ambayo yanahusisha Sh. Bilioni 11 na zaidi.
Chalamila amezitaja chunguzi hizo kuwa ni katika mkataba wa upangishaji wa jengo la Ngorongoro Tourism Center kwa kodi ya Sh. Bilioni 7.96 ambapo mpangishwaji wa jengo hilo alipangishwa chini ya bei iliyoelekezwa na bila kupata ridhaa ya Bodi ya Wakurugenzi.
“Chunguzi pia zimebaini kuwepo kwa vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha wa shilingi bilioni 4.2 kwa watumishi wa kitengo cha Agency Banking cha Benki ya CRDB kutoka kwa Mawakala Wakuu (Super Agency) ili wasiwasitishie mikataba yao ya uwakala.
“Vitendo vya rushwa na uchapishaji wa fedha kwa kushirikisha watumishi wa benki na watuhumiwa wengine ambapo bilioni 2.35 zilichepushwa na Maofisa wa Benki ya ABC kupitia miamala iliyofanyika na kurejeshwa (Teller Reversal Entries), miamala ya kutuma pesa kutoka kwenye account kwa njia ya simu (mobile banking transfers), kuruhusu miamala iliyopitiliza iliyofanywa kwa kupitia huduma ya kadi ya malipo ya kabla (Card Over drawn in Connection with pre-paid card services),” amesema
Amesema vitendo vya rushwa vilivyofanywa na kampuni ya NatGroup Limited kwa kushirikiana na watu wengine kama dhamana wakati wa kuchukua Credit Bond yenye thamani ya Sh. Bilioni 2.3 kutoka First Assuarence kwa lengo la kupata uwezo wa kununua petroli kwa njia ya mkopo kutoka kampuni ya usambazaji mafuta ya United Petrolium Limited.