NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa maandalizi ya mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utakaofanyika Januari 27 na 28 mwaka huu hapa nchini, yafikia asilimia 95.
Mkutano huo kushirikisha wakuu wa Nchi takribani 54, Mawaziri wa Fedha na Nishati kutoka barani Afrika na Marais wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Viongozi wa Jumuia ya Ulaya na Jumuia ya umoja wa Afrika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akikagua ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao mkutano huo utafanyika hapo, amesema kazi zinazoendelea kwa sasa ni kukamilisha ukarabati wa ukumbi huo kutokana na ugeni ambao unakuja nchini na ili uendane na hadhi ya mkutano huo lazima ukarabati huo ufanyike.
Amesema mbali na ukarabati huo wanaendelea na zoezi la usajili na udhibitisho wa wakuu wa nchi pamoja na wageni wengine ambao watakuja kwaajili ya ushiriki wa mkutano huo,huku wakiendelea na ukarabati wa maegesho ya magari barabarani na kuweka matangazo maeneo mbalimbali kuhusu mkutano huo.
”Naushukuru sana uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kubeba wajibu huo wa kubland mkutano huu na kuhakikisha mkutano unafanyika kama ulivyokusudiwa.
”Tanzania kama mwenyeji wa mkutano huu ambao kwa kiasi kikubwa unatokana na demokrasia nzuri ambayo Rais Samia Suluhu Hassan anayofanya imesaidia kuimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa kuhusiana na mataifa mengine na kupelekea benki ya Dunia na Maendeleo ya Afrika kuichagua Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano huu,”amesema
Hata hivyo amesema iliyosababisha Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni kutokana na kupiga hatua katika sekta ya nishati kwa kuweza kupeleka umeme hadi vijijini na vitongojini.
Biteko amesema kutokana na ukweli wa nchi ya Tanzania kuwa mojawapo iliyofanya vizuri barani Afrika katika sekta ya nishati ndio sababu nyingine iliyochangia mkutano huo kufanyika nchini.
”Mkutano huu utakuwa na faida mbalimbali ikiwemo kuongeza kwa kasi kiasi cha watanzania wote kuunganishwa na umeme hadi kufikia Milioni 13.5 kwani bila mpango huu Tanzania hadi kufikia 2030 ingeweza kuunganisha watu Milion 5.5,” amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uongozi wa Dar es Salaam umeweza kujipanga kikamilifu katika kuandaa maeneo mbalimbali ikiwemo ya tiba pamoja na eneo la wageni kufanya mazoezi pindi watakapokuwepo katika mkutano huo.