NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
SHULE ya Kimataifa ya Arusha Meru (AMIS) ilifanya onesho la elimu, ujuzi na ubunifu lililovutia wanafunzi kutoka shule mbalimbali za kimataifa.
Hafla hiyo ilifanyika Arusha, Novemba 1, 2024, shuleni hapo jijini Arusha ilijumuisha miradi ya kisayansi inayolenga kutatua changamoto za kijamii na mazingira, na kuonesha ubunifu wa wanafunzi.
Katika onesho hilo, wanafunzi wa shule ya AMIS walionyesha miradi mbalimbali, ikiwemo utengenezaji wa biodiesel kutoka mafuta ya mboga.
Wanafunzi Gaspar Chacha, Shedrack Mbasha, na Shawn Antony walielezea jinsi walivyotumia potasiamu hydroxide na methanol kuunda nishati mbadala inayopunguza uzalishaji wa hewa chafu. “Biodiesel ni njia nzuri ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Chacha.
Wanafunzi wengine walionesha ubunifu wao kwa kutumia piezoelectric, vifaa vinavyoweza kubadilisha mitikisiko kuwa nishati. Presley Meleczedec, Patricia, na Tracey walifafanua jinsi wanavyoweza kukusanya nishati kutokana na mitikisiko ya watu katika maeneo ya umma. “Hii itasaidia katika kuunda nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyotokana na mafuta,” walisema.
Miradi ya ajabu pia ilitolewa na wanafunzi wa shule ya Mtakatifu Jude,Aisha Saidi, Neema Charles, na Sabrina Mohamed walitengeneza barabara kwa kutumia chupa za plastiki.
Walisema, “Tumejenga barabara hii ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha miundombinu vijijini.” Hii ni hatua muhimu katika kutatua tatizo la taka za plastiki na kuboresha maisha ya watu.
Wanafunzi Jasem Abdallah, Aarush Gada, na Faraj Mohamed walikamilisha mradi wa gari dogo la umeme. Jasem alisema, “Tumetumia chuma kutengeneza injini ya Honda ambayo inaweza kuendeshwa na uzito wa chini ya kilo 70.” Gari hilo lina uwezo wa kukimbia kilomita 140 kwa saa na linatumia lita tatu za mafuta kwa kila kilomita 180.
Mkurugenzi Mtendaji wa AMIS, Dk. Ishaan Ahmad Khan, alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika elimu. “Tunataka kuwapa wanafunzi fursa ya kuonyesha uwezo wao katika masuala ya kisayansi. Onyesho hili ni njia nzuri ya kuwapa motisha na kuwajengea uelewa mzuri wa sayansi,” alisema Khan.
Kaimu Mkuu wa shule, Mustapha Omary Nassor, aliongeza kuwa elimu ya sayansi ni muhimu kwa maendeleo ya jamii. “Lazima tuweke juhudi katika kukuza uelewa wa sayansi ili wanafunzi wetu waweze kutatua matatizo yanayowakabili,” alisema Nassor.
Onesho hilo lilihusisha jumla ya miradi 300 kutoka shule mbalimbali, na kushirikisha wazazi na jamii katika kuhamasisha elimu. Wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao na kupata mawazo mapya katika uwanja wa sayansi.
Hafla hiyo pia ilijumuisha zawadi kwa washindi wa miradi bora, ikiwa ni njia ya kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi. “Tunatarajia kuona matokeo chanya kutokana na miradi hii katika siku zijazo,” alisema Khan.