NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
KONGAMANO kuhusu Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Mpango wa Ufadhili wa Sekta ya Afya yanafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha kuanzia Oktoba 29 na 30 2024 na 31 Oktoba na 01 Novemba 2024.
Matukio hayo mawili yatakayofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) siku ya 30 Oktoba 2024 yamekusanya wataalamu kutoka sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kujadili mikakati inayofaa kutumiwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuboresha huduma za afya kwa wote.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wabia wa maendeleo imeshiriki uratibu wa maandalizi ya matukio hayo muhimu ambapo Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Mpango wa Ufadhili wa Sekta ya Afya, kufanyika kwake ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kikao chao kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2024.
Aidha, mdahalo huo ni utekelezaji wa maazimio ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika waliyoyatoa katika Mkutano wao uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Julai 2019.
Katika siku yake ya kwanza, washiriki wa kongamano hilo walipata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na watalaam wa afya. Kabla ya mada hizo kuanza kuwasilishwa, zilitanguliwa na hotuba fupi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu na Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Afya, Amoury A. Amoury
. Watalaamu hao waliwambia washiriki madhumuni ya kongamano hilo na matokeo yanayotarajiwa na dira ya mpango wa bima ya afya kwa wote nchini Tanzania.
Mada nyingine zilizowasilishwa katika siku ya kwanza ni pamoja na Kugharamia Mfumo wa Afya kwa Wote: Kuangalia kwa kina mikakati ya kibunifu kwa ajili ya Upatikanaji Endelevu wa Fedha; (Financing Universal Health: Exploring Innovative Strategies for Sustainable Funding in Tanzania); Nafasi ya Teknolojia na Ubunifu katika Kuboresha Ufanisi na Upatikanaji wa Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote; (Role of Technology and Innovation in Improving Access and Efficiency in Universal Health Insurance); na Enrolment and Re-enrolment Strategies – what works and what does not work.
Wizara inawakilishwa na timu ya watalaamu katika kongamano hilo inayoongozwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Mhandisi Abdillah Mataka na siku ya ufunguzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Denis Londo (Mb) atashiriki hafla ya ufunguzi ya matukio hayo.