NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kufikia Dola za Marekani Milioni 5,413.6 mwishoni mwa Septemba 2024 kutoka dola za Marekani Milioni 5,345.5 Juni 2024.
Hayo yamesemwa na Gavana wa BoT, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Fedha (MPC) ya benki hiyo, Emmanuel Tutuba kupitia taarifa yyake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Oktoba 3, 2024.
Gavana Tutuba amesema akiba hiyo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya miezi minne ambayo inaendana na lengo la nchi.
Amesema upatikanaji wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asili kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba.
“Mauzo ya mazao ya chakula hususan mahindi na mchele kwenda nchi jirani pia yanatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni,” amesema Gavana Tutuba
Aidha amesema kupungua kwa uingizaji wa mbolea na kupungua kwa bei za bidhaa za mafuta ya nishati kunatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.
“Matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha. Benki Kuu itaendelea kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu katika soko la ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania,” amesema
Hata hivyo amesema mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha ikiwa ni takriban asilimia 17.1 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 sawa na ukuaji uliofikiwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2024.
Amesema ubora wa rasilimali za benki uliendelea kuongezeka ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 3.9 mwezi Agosti 2024, kutoka asilimia 5.1 katika mwezi kama huo mwaka jana.
.