- VEMA kesho iwe bora, kuipita jana yangu,
Ya leo yanayokera, yasiwe ya kesho yangu,
Nimeshapata hasara, ijayo faida kwangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Ilikuwa mbili jii, ya kule kwa ndugu zangu,
Tukafika tatu jii, niliona simu yangu,
Tunatamba nne jii, Wafrika nao Wazungu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Sasa kuna tano jii, kwa hao rafiki zangu,
Nisibaki nchi hii, jii zile za wenzangu,
Hamu yangu niitii, nami nipae kivyangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Mamlaka nimeona, zinacheza mechi yangu,
Safari fululizana, saa zote ni za kwangu,
Lami zinapandiana, na reli ni raha kwangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Giza ni la zama zile, wala sasa si la kwangu,
REA hapa hata kule, wanatibu kiu yangu,
Na kila mahali shule, nanoa ubongo wangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Pembejeo kijijini, yabaki bidii yangu,
Ruzuku serikalini, imegusa moyo wangu,
Sasa na mimi kazini, nipate mazao yangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Unataka nifikia, ufike nyumbani kwangu,
Bofya kwa kuangalia, anwani makazi yangu,
Kupotea shaishia, siyo hizi zama zangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Punde gesi asilia, takuwa nishati yangu,
Nitumie kupikia, kusukuma gari yangu,
Dola kuzihitajia, iwe si lazima kwangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Kwa hamu nasubiria, treni kwa raha zangu,
Niweze kusafiria, kwa zote safari zangu,
Si njiani kulalia, nikwamishe mambo yangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Urusi na Ukraine, wauchosha mwendo wangu,
Ile mipango mingine, kuongeza pato langu,
Imekwama nisivune, mazuri matunda yangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Mvurugo wa ugavi, sasa ni kikwazo kwangu,
Kwangu sasa ni ugomvi, na hawa wateja wangu,
Wadhani miye mlevi, huku kuchelewa kwangu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Siku zote duniani, sibaki pale mwenzangu,
Vema toka kwa uduni, upate fikia mbingu,
Ili uwe furahani, umsifu wako Mungu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu. - Nina neno moja kwako, nakuombea mwenzangu,
Utoke huko uliko, kama umefungwa pingu,
Fika kwenye nuru huko, ulipate lako fungu,
Mwendo wangu uwe ule, toka chini kwenda juu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602