NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Selemani Jafo (Mb) ametembelea Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika kilele cha Maonesho ya Wakulima na Wafugaji maarufu kama Nane Nane jijini Dodoma na kuhimiza kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa wakulima.
Akizungumza na Wataalamu wa WMA wanaoshiriki Maonesho hayo, Jafo amepongeza maandalizi mazuri yaliyofanyika na kusisitiza kuwa elimu ya vipimo iendelee kutolewa kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla.
“Elimu ya vipimo ni muhimu sana hivyo hata baada ya Maonesho muendelee kuwaelimisha wananchi,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kiula, amesema Wakala hiyi itaendelea kutoa elimu ya vipimo kwa wananchi kwa siku mbili zaidi katika Maonesho ya NaneNane kufuatia agizo la Mgeni Rasmi, Rais Samia Suluhu Hassan alilotoa wakati akifunga Maonesho husika yaliyoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.
Aidha, Kiula ameongeza kuwa WMA itaendelea kutoa elimu kupitia kampeni mbalimbali nchi nzima katika kuhakikisha wananchi wote wanapata uelewa kuhusu matumizi ya vipimo sahihi pamoja na manufaa yake.