NA DANSON KAIJAGE,DODOMA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa Wizara ya hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeingia makubaliano na Magereza zote nchini kwa lengo la kuwataka na kuwahamasisha kutumia gesi asilia kwa lengo la kuacha matumizi ya nishati chafu inayochochea uharibifu wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa muda mfupi baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Nishati na taasisi zake kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema Wizara ya Nishati imejipanga ipasavyo kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024 – 2034) ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kufikisha lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi katika kipindi cha miaka 10.
“Tunafanya kazi na Taasisi zinazolisha watu wengi mfano Magereza, hivyo wizara ya Nishati kupitia REA tumeingia makubaliano na magereza zote kwamba watawekewa mitungi mikibwa pamoja na kuwekewa Majiko maalumu yanayotumia mkaa ambao hauathiri Mazingira Wala hautoi moshi na haya yote yanafanyika kwa lengo la kuachana na matumizi ya nishati chafuzi inayochangia uharibifu wa mazingira”. ameeleza.
Aidha, Mhandisi Mramba ameeleza kuwa jitihada za serikali ya awamu ya sita kwa uongozi imara wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuelekea kwenye matumizi ya Nishati safi ya kupikia Kwa kushirikiana na wafanya Biashara,wabunge pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi.
‘Katika Sekta ya Nishati inafungamanisha Sekta nyinginezo ikiwemo Madini, Maji, Kilimo na Mifugo ambapo katika Mifugo vinyesi vya wanyama hutumika kuzalisha nishati kwa ajili ya matumizi mbalimbali”. amesema
Serikali ya Tanzania kupitia Sera mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa inatambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo ameeleza kuwa itakapo tumika nishati safi kama vile gesi asilia itasaidia kukuza uchumi wa taifa ikiwa ni pamoja na kurahisisha utendaji wa kazi kuliko ilivyo sasa.
Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kupambana kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kwa kushirikiana na Kampuni mbalimbali ambazo zinazalisha bidhaa kwa lengo la kurahisisha utendaji wa kazi.