NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amezindua Jengo Mtambuka la Mafunzo liliopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kuridhia ombi lililotolewa na Mkuu wa Chuo hicho Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba la kutaka Jengo hilo liitwe jina la Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati akitoa salaam kwa wanajumuiya wa SUA katika uzinduzi huo, Mhe. Rais amesema amekubali ombi hilo lakini akatoa ombi la kutaka jengo lingine linalojengwa na Chuo hicho litakapokamilika basi lipewe jina la Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda kutoka na kazi nzuri anayoifanya ambayo matunda yake yanaonekana kwa taifa ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa majengo.
“Mimi nimeridhia jengo hili liitwe Samia lakini nimeambiwa hapo nyuma kuna majengo mengine yanajengwa na jengo moja lipo kwenye hatua nzuri niwaombe likimalizika liitwe Chibunda maana amefanya kazi nzuri sana sana, hongera Prof. Chibunda pamoja na Menejimenti yote ya SUA”, amesema Rais Samia.
Aidha Dk. Samia amekitaka Chuo Kikuu cha SUA kuendelea kulitunza jengo hilo ili liendelee kuwa na viwango vyenye ubora wa kimataifa na kuwavutia wanafunzi kutoka nje ya Tanzania.
Akitoa taarifa ya Chuo hicho Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema Chuo cha SUA ni kati ya Vyuo vikuu vinavyonufaika na mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kuishukuru Serikali kwa kukitengea Chuo Sh. Bilioni 73.6 kupitia mradi huo.
Amesema kwa sasa Mradi upo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo kwa upande wa miundo mbinu mradi huo utasaidia kujenga majengo 9, majengo mawili katika Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo Katavi, majengo mengine 2 Kampasi ya Solmon Mahlangu na majengo 5 Kampasi ya Edward Moringe Sokoine.
Aidha katika kuimarisha mafunzo ya ujasiriamali Prof. Chibunda amesema Chuo hicho kinaendesha Kituo Atamizi kwa vijana katika kilimo ili kuwajengea uwezo wanafunzi na wadau wengine katika masuala ya kilimo biashara ambapo kwa sasa Chuo kina vitalu 91 na vitalu 20 vya kilimo cha nje na tayari wameatamia na kuhitimisha jumla ya wanafunzi 347 katika mafunzo hayo.
“Chuo chetu pia kimeanzisha mpango wa kuwawezesha wanafunzi kufungua kampuni za ujasiriamali, kupitia kampuni hizo wanafunzi huja na bunifu mbalimbali ambazo ukitangaza Chuo kitaifa na kimataifa, juhudi hizo zimeanza kutoa matunda ambapo kampuni moja ya wanafunzi watano wa Chuo chetu wanamiliki Kampuni ya Mnyama Digital Limited na tayari wamejishindia tuzo ya kimataifa ya ubunifu bora wa vijana wenye biashara zinazochipukia”amesema Prof. Chibunda.