NA DANSON KAIJAGE, DODOMA
AKINA Mama wenye watoto wenye umri wa kunyonya wametakiwa kuwanyonyesha watoto wao kwa umri wa miaka miwili au zaidi kwa lengo la kuwafanya wanao kupata afya njema.
Rai hiyo imetolewa na Ofisa Lishe kutoka Wizara ya afya Elieth Rumanyika alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu juu ya umuhimu wa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama.
Rumanyika amesema kuwa ni muhimu kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa mtoto kuanzia siku 0 hadi miezi sita bila kumpatia chakula chochote kwa umri huo.
Pia ameeleza kuwa mtoto akifikisha umri wa miezi sita mtoto aendelee kunyonya maziwa ya mama huku akipewa chakula kisaidizi hadi kufikia miaka miwili kamili au zaidi.
Akizungumzia lishe huyo ameeleza kwamba kuna faida kubwa ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwani kwa kufanya hivyo ni pamoja na kumjenga mtoto kiafya kutokana na maziwa ya mama kuwa na virutubisho vingi.
Katika hatua hiyo amesema kuwa Tanzania ni kati ya nchi duniani ambayo kwa sasa hipo katika wiki ya unyonyeshaji ambayo kilele chake ni Agosti 7, 2024 na kwa kuzingatia hilo Wizara inawahamasisha wamama wote wanaonyonya kunyonyeshwa kwa usahihi zaidi.
“Nataka kuwahamasisha akina mama wanaonyonyesha kuhakikisha wanawanyonyesha watoto wao kwa usahihi kabisa,Mfano mtoto kuanzia siku sifuri hadi miezi sita anatakiwa kunyonya maziwa ya mama bila kupewa kitu chochote.
“Mtoto akifikisha miezi sita na kuendelea anatakiwa kunyonya hadi miaka miwili na zaidi huku akipewa chakula kisaidizi na siyo maziwa ya mama yageuzwe kuwa kisaidizi”amesema Rumanyika
Sambamba na hilo amehimiza akina mama wanaonyonyesha kutoyakamua maziwa yao ya toka ajifungue hado siku tatu kwa kujijengea imani potofu kwa kudanganyana kuwa maziwa hayo ni mabaya na hayafai.