NA ASHRACK MIRAJI,DAR ES SALAAM
TAASISI isiyo ya kiserikali ya Utulivu kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kufanya matembezi maalumu ya Utulivu Julai 20 mwaka huu huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitarajiwa kuwa Mgeni rasmi.
Matembezi hayo yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya farasi (Green Grounds) vilivyopo Oysterbay Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano na Wanahabari mapema Julai 18,2024 Katibu Mkuu wa Taasisi ya UTULIVU SPACE , Mboni Kibelo amesema kuwa wamelenga kuandaa matembezi hayo ikiwa pia ni hamasa kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za Utulivu zinazotarajiwa kufanyikaSeptemba 14 mwaka huu.
”Sisi kama Utulivu tuligundua kuwa nchi yetu imebarikiwa vitu vingi vizuri lakini maarufu sana kwa ukarimu wa watu wake. Kwa kulitambua hilo tumeamua kuandaa jukwaa hili kwaajili ya kuyaenzi yale mazuri yaliyoasisiwa na baba wa taifa letu miaka ya nyuma kwenda kwa jamii ya kizazi cha sasa. Hivyo tumeamua kuja na Jukwaa hili la Utulivu kwaajili ya kufurahia Utulivu na Amani tulionao kama Taifa” amesema Kibelo.
Kwa upande wa wizara ya Utamaduni Sanaa na michezo, Ofisa Mwandamizi wa Sanaa Abel Ndaga naye amesema kuwa wameamua kushirikiana na Taasisi ya Utulivu kuandaa matembezi hayo ikiwa ni kuunga mkono kwa juhudi zilizofanywa na Waasisi wa Taifa hili katika kuwaunganisha watanzania na kuwa kitu kimoja .
”Sisi kama Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tumeamua kushirikiana na ndugu zetu wa Utulivu katika kuunga mkono yale ambayo viongozi wetu waliyaanza katika kutuunganisha watanzania kupitia Sanaa na michezo mbalimbali” amefafanua Ndaga
Aidha Ndaga ameongeza kwa kuwaomba watanzania kushiriki katika matembezi hayo kwani hayana ada ya ushiriki na pia kutakuwa na mfululizo wa shughuli mbalimbali za kiburudani zitakazokuwa zikiendelea siku hiyo.