NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
OFISA Lishe na Muuguzi Mbobezi Kitengo cha Wagonjwa Mahututi kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), Zainabu Tindi amesema mtu yeyote aliye katika hatua za kupunguza uzito wa mwili anatakiwa kupunguza si chini ya kilogramu tatu kwa mwezi .
Sambamba na hilo mtu atakayejipunguza uzito ghafla anaweza kupata tatizo la nyama zake za mwili kuuma, kuonekana mzee na wakati mwingine mwili wa ndani kushtuka.
Tindi amebainishwa hayo wakati akizungumza na Demokrasia kwenye banda la MOI lililopo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema mafuta ya mwili yanapaswa kuondoa kidogokidogo hivyo kwa yeyote atakayepungua ghafla nyama lazima zimuume na wakati mwingine kuonekana mzee hivyo watu wake wa karibu kuishia kumshangaa.
“Kama unataka kupungua uzito unatakiwa kuuandaa ubongo wako kwa kuuambia kuwa sasa nataka kupungua, andaa pia moyo na nafsi, ukiwa na roho ndogo utoweza kupungua uzuto, jambo hili linahitaji watu waliotayari kukataa uzito uliopitiliza,” amesema na kuongeza
“Tuseme ukweli vyakula vyetu ni vitamu mnoo alafu vina radha hivyo kupungua uzito si jambo rahisi hata kidogo, anayetaka kufanya jambo hilo anatakiwa kujipanga kweli kweli kwa kuandaa hata nafsi na moyo wake,” amesema
Amesema ili mtu aweze kupungua anaweza kuweka malengo , mwezi huu Julai kwamba hadi mwakani mwezi kama huo walau awe amepungua kilo 8 hadi 10 na kwamba ni muhimu kwenda kidogo kidogo ili hata wale wataokuangalia wanaona umepungua kidogo.
Amesisitiza kuwa katika kitengo chake amekuwa akipata kesi nyingi juu ya uzito wa watu kuzidi, yaani uwiano wa urefu na uzito haviendani na kwamba hilo kwa sasa limeendelea kuwa tatizo kubwa nchini.
“Kupunguza uzito siyo kitu cha siku moja au mbili, ni vizuri watu wakapima kwanza uzito na urefu ili kujua uwiano wa uzito na urefu wao ni ngapi, kwa kawaida kabisa tunaotakiwa kuwa nao ni 19.5 hadi 24 kwa yeyote yule inatosha na ni salama,” amesema