NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha kwa wakati miradi mitatu wanayoitekeleza ukiwemo wa Samia Housing Scheme (SHS) uliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava mara baada ya kutembelea miradi huo na mingine miwili ambayo ni Kawe7 11 uliyopo Kawe na Morocco Square yote ikiwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miradi hiyo, Mzava amesema kuwa NHC kwa sasa hawana kisingizo tena cha kutokamilisha miradi hiyo kwani tayari fedha zimeshatolewa.
“Kama kamati hatutamani kuona miradi hii inasimama au kwenda kwa kusuasua kwa sababu kisingizio kilikuwa ni fedha lakini tayari Rais ameshatoa fedha hivyo tunawaomba NHC wawasimamie wakandarasi wakamilishe miradi hii mikubwa kwa wakati,”
Aidha Mnzava ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe vijijini amesema kuwa
kamati hiyo imebaini kuwa kazi hiyo isingefanyika vizuri kama siyo nia, moyo, mtazamo na maono ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hasa kutoa kibali kwa NHC kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tunampongeza Rais kwa kazi hiyo nzuri ya kuruhusu NHC kupata fedha ili kuendelea na miradi, pia tunalipongeza Shirika letu ya nyumba kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii,” amesema
Amesema kamati imefurahi na kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi hiyo mitatu kwani katika miradi hiyo mmoja ni wa muhimu unakwenda kuacha alama ya Rais Samia.
Hata hiyo alisema kuwa miradi miwili ambayo ni Morocco Square na Kawe 711 ilisimama kwa muda mrefu kutokana na maelekezo ya Serikali ya kulitaka shirika hilo liweze kufanyakazi vizuri hasa katika kutafuta fedha za kutekeleza miradi.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema wanamahukuru Rais Samia kwa kuridhia miradi hiyo kuendelea kwakuwa hapo awali ilisimama kwa muda kupisha mambo ya kiserikali.
Amesema mradi wa Morocco Square umeshakamilika kwa asilimia 99 na tayari majengo yaliyopo hapo yameshachukuliwa na wapangaji na wanunuzi kwa asilimia 90 na hiyo ni ishara kwamba miradi sasa inafanyavizuri.
“Tutaendelea kusimamia maelekezo ya Rais Samia kuhakikisha kwamba miradi hii inamalizika kwa wakati na inaleta tija kwa wananchi na nchi kwa unumla,” amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah amesema shirika linaendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa huo SHS ambapo utekelezaji wake unaendelea.
Amesema mradi huu wa SHS ni mradi wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anayofanya Rais Samia ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora nchini.
Alisema asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa katika mkoa wa Dar es Salaam ,asilimia 20 mkoa wa Dodoma na 30 mikoa mingine.
“Mradi huu wa SHS utakuwa na nyumba 5000 ambapo utatekelezwa kwa awamu na utagharimu kiasi cha sh.bilioni 466 sawa na dola za kimarekani milioni 200, katika kuendeleza mradi huo,maandalizi ya ujenzi wa mradi SHS wenye nyumba 100 jijini Dar es Salaam na nyumba 560 eneo la Kawe awamu ya pili yanaendelea kukamilishwa,” amesema na kuongeza
“Nyumba 560 zinaendelea kujengwa katika eneo hilo ambapo hadi kufikia Juni 30,2024 ujenzi wa nyumba hizo umefikia asilimia 65.
Mradi huu wa Kawe utagharimu kiasi cha sh.bilioni48.27 na hadi sasa takribani kiasi cha sh.biliioni 21.88 zimeshatumika,” amesema
Amesema mauzo ya mradi huo yamefikia asilimia 100 na tayari Shirika limepokea malipo ya awali ya kiasi cha sh.bilioni 31.2 na kiasi kilichobaki ni Sh.Bilioni45.5 zinaendelea kukusanywa.
Akizungumzia mradi wa Morocco Square alisema umekamilika kwa asilimia 99 na shughuli za upangishaji tayari umeanza kwa baadhi ya maeneo ikiwemo hoteli yenye vyumba 81 umekamilika na eneo la ofisi za biashara upangishaji unaendelea kukamilika.
Aidha alisema jengo lenye nyumba za makazi 100,tayari nyumba 71 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobaki yanaendelea.
Alisema hadi sasa katika nyumba za makazi na biashara zilizouzwa shirika limekusanya kiasi cha sh.bilioni 30 na kiasi cha sh.bilioni 35.9 kinaendelea kukusanywa huku eneo la maduka limeshapangishwa kwa asilimia 98 na kwasasa upangaji wa bidhaa unaendelea ili kufungua maduka hayo mwezi julai mwaka huu.
Akizungumza mradi wa Kawe 711,alisema mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 40 ambapo unanyumba 422, pamoja na sehemu za biashara ambao ulianza November 2014 na ulisimama 2018.
Alisema mradi unatekelezwa na mkandarasi Estim Construction Company Limited kwa gharama ya sh.bilioni 169.9 na kwa sasa mradi unatarajia kukamilika Aprili 2026.