NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania na Guinea Bissau imepanga kushirikiana katika kukuza biashara hasa ya zao la korosho na kuongeza tafiti za kukuza uzalishaji wa zao hilo ili kuliongezea thamani.
Aidha Rais Samia amesema nchi hizo mbili zimepanga pia kushirikiana katika ukuzaji wa amani na usalama barani Afrika, ukuzaji wa biashara na uwekezaji, Elimu, afya pamoja na uchumi wa buluu.
Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 22, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mazungumzo baina yake na Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
“Tanzania na Guinea Bissau ni wazalishaji wakubwa wa korosho kwahiyo hilo ndilo eneo ambalo tumesema tuanze ushirikiano na hasa kufanya utafiti na kuongeza thamani ya mazao yetu.
“Eneo lingine ni maeneo huru ya uwekezaji ambapo baada ya kumaliza leo Rais Embalo ataangalia maeneo yetu ambayo ni EPZA na Reli ya Kisasa ya SGR ili kuona mfano halisi jinsi miundombinu inavyounganisha nchi zetu hizi mbili,” amesema Rais Samia
Rais Samia amesema pia wamekubaliana kushirikiana na nchi zingine za Afrika katika kuhakikisha bidhaa za kilimo za Tanzania na Guinea Bissau zinapata bei nzuri kwa kutengeneza umoja katika soko la dunia.
Aidha amesema bara la Afrika lipo mbioni kuhakikisha eneo huru la biashara linafunguka lengo likiwa ni kukuza zaidi kiwango cha biashara kati ya nchi za Afrika.
“ Kuanzishwa kwa eneo hili pia kutachochea ukuaji wa viwanda, uongezaji wa thamani wa mazao yetu na kuleta ajira kwa vijana hivyo tumesema eneo hili huru la biashara tunalitumia ipasavyo,” amesema
Hata hivyo amesema Tanzania na Guinea Bissau zina maeneo makubwa ya Pwani hivyo watashirikana kwenye masuala ya uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi, utalii kwenye fukwe na usafirishaji baharini.
“Pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya tishio la ugaidi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya” amesema
Naye Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo’ amesema Tanzania na nchi yake zikifanya kazi kwa pamoja zinaweza kuwa na amani ya kudumu na ustahimilivu wa kisiasa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha amesema wanawakaribisha sekta binafsi nchini Guinea Bissau kuwekeza kwani nchi hiyo ni lango muhimu la kuingia nchi zingine za Magharibi hasa kupitia eneo huru la biashara Afrika.