* Ni kupata fursa lukuki kutoka serikalini
*Kuepuka mivutano na Serikali
* Ada ya usajili ni Sh.800,000 kwa mtaji wa Sh.Mil.10/-
*Kupata usajili ni saa moja hadi 72
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
IMEELEZWA kuwa miongoni mwa faida za kusajili Viwanda ni pamoja na kupata fursa za vivutio vinavyotolewa na Serikali katika nyakati tofauti ikiwemo mafunzo.
Licha ya kupata fursa ambazo Serikali inatoa kwa nyakati fulani pia mmiliki wa kiwanda anaposajili anakuwa ametii sheria bila shuruti inayosaidia kupunguza mivutano isiyokuwa ya msingi baina ya pande hizo mbili.
Hayo amebainisha leo, Juni 19, 2024 mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Leseni wa Wakala Usajili Leseni za Biashara (BRELA), Andrew Mkapa wakati akiwasilisha mada inayohusu Leseni za Viwanda kwa Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaoudhuria mafunzo yenye lengo la kuwaongezea uelewa namna ya kuripoti taarifa na shughuli zinazotolewa na Brela bila kupotosha umma.
“Mwekezaji anaposajili/ kurasimisha kiwanda, Serikali inapata takwimu sahihi ya viwanda vilivyopo nchini na aina ya bidhaa ambazo inazalishwa ili kuweka mipango stahiki kwa maendeleo yao na mapato ya Serikali kuongezeka yanayotokana na ada ambayo ni sawa na gharama za kuendesha huduma hiyo” amesema.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa sheria iliyopo, ada kwa viwanda vikubwa na kati wanatakiwa kulipa Sh. 800,000 kwa uwekezaji unaozidi milioni 100 na kupatiwa leseni.
Mkapa ameongeza kuwa uwekezaji wa Sh.Mil.5/- atalipiwa Sh. 10,000, unaozidi Mil. 5, analipiwa Sh.50,000 na unaozidi Sh.Mil.10/-, atalipia Sh.100,000 na wote watalipa ada mara moja tu na kupewa leseni ya kudumu kwa uwekezaji wa viwanda vikubwa na kati, viwanda vidogo wanapewa cheti cha usajili.
Mkapa ameongeza kuwa kutokana na kuwa na mfumo madhubuti ambao Brela imeutengeneza unaoitwa ORS , Mmiliki wa kiwanda anaweza kufanya usajili popote halipo na kwa urahisi unaonzia kupitia mfumo wa Serikali unaoitwa the TNBP ( www.business.og.tz ).
Ameongeza kuwa maombi yote ya usajili yanachukua kuanzia saa moja hadi siku tatu kulingana na changamoto zitakazojitokeza wakati mchakato wa usajili.