NA MWANDISHI WETU,MBEZI DAR ES SALAAM
MWANAFUNZI wa darasa la sita Shule ya Msingi Malamba Mawili Mbezi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Alec Michael (12) amekutwa amefariki huku mwili wake ukiwa na sare za shule ukining’inia kwenye mti ulio jirani na makazi ya watu leo Mei 22, 2024 saa moja asubuhi.
Demokrasia ilifika eneo la tukio majira ya saa moja na nusu asubuhi na kukuta umati wa watu huku mwili wa mwanafunzi huyu ukiwa unaning’inia kwenye mti huo.
Kwa mujibu wa Mary Mbuya jirani wa lilipotokea hilo aliieleza Demokrasia kuwa hakujua kilichotokea hadi binti yake alipokuja kumuamsha kwamba kuna umati wa watu nje ya nyumba yake.
Mbuya alieleza kuwa baada ya kutoka nje alikutana na umati huo na mwili wa mwanafunzi huyo na alichokifanya ni kumpigia simu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malamba Mawili Evetha Gaspar ili kupata msaada zaidi wa kumtambua mwanafunzi huyo.
” Tukio hili limenistua sana ,limenisikitisha sana na nilichokifanya ni kumpigia simu mwenye eneo lake ( baba Khalifa) pamoja na Askari wa jirani ambao walifika kwa haraka “alieleza Mbuya.
Naye Gaspar Mwalimu Mkuu wa shule ya Malamba Mawili alipokuwa anasoma mwanafunzi huyo aliimbia Demokrasia kuwa anamfahamu Marehemu na alisema anashangaa kuona kilichotokea.
” Alec hakuwa na tatizo wala historia yeyote ya magonjwa na alikuwa ni mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa darasani hivyo sielewi kilichosababisha mauti yake hivyo naliachia Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake”alieleza kwa masikitiko makubwa
Kwa upande wake Mwanafunzi mwenzake ambaye hakutaka jina litajwe alisema amemfahamu Alec kwa muda mrefu na hadi jana walikuwa wote akiwa na kamba ambayo hakujua ni ya nini…
“Tulikuwa na Alec jana akiwa na kamba ya ambayo binafsi sikujua ni ya nini,nilitamani kumnyang’anya lakini alikataa..naumia sana lakini ndio hivyo rafiki yangu leo tunamkuta hapa akiwa amefariki..” alieleza mwanafunzi huyo.
Hadi Demokrasia inaondoka eneo la tukio Askari walikuwa wakiendelea kuuondoa mwili wa Mwanafunzi huyo sambamba na kupata maelezo kutoka kwa Walimu na mama wa marehemu Alec ambaye alikuwepo eneo hilo.
Taarifa zaidi za tukio hili zitakujia kadri Demokrasia itakavyozipokea kutoka kwa Jeshi la Polisi na familia.