NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wananchi wa mkoa wa Arusha.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira Vijana na Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya Dk. Samia Suluhu Hassan Outreach Services katika maonesho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi yanayofanyika viwanja vya General Tyre jijini Arusha.
Ndejembi alisema JKCI imekuwa ikifanya vizuri katika kutoa huduma za matibabu ya moyo nchini na kuwa kimbilio kwa wananchi wengi wenye magonjwa ya moyo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, JKCI naijua vizuri kutokana na huduma zake za kipekee inazozitoa za matibabu ya moyo hapa nchini”, alisema Ndejembi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la JKCI Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dk. John Mduma alishukuru kwa kupatiwa huduma za uchunguzi wa afya na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya.
“Nawashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa kunipa nafasi ya kupima afya yangu lakini hamkuishia hapo bali mmeweza pia kunipa elimu kuhusu mfumo bora wa maisha”, alisema Dk Mduma
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule ya msingi Highridge Adam Washokera alisema alipofika katika banda hilo na kupatiwa huduma aliona kuna fursa ya kuwaleta wanafunzi wa shule yake kujifunza kuhusu moyo kwani ni vitu ambavyo wanafunzi wanajifunza darasani.
“Baada yakufika katika banda hili na kupatiwa huduma niliona fursa ya kuwaleta wanafunzi wa darasa la nne na la saba kujifunza kuhusu moyo kutoka kwa daktari bingwa wa moyo kwani daktari anaujua moyo vizuri hivyo watoto wamepata elimu kwa vitendo”, alisema Washokera
Washokera alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa na ndoto ya kuwa madaktari hivyo wakisogezwa karibu na watu wa ndoto zao wanapata motisha zaidi kusoma na kufikia ndoto zao.
Naye mwananfunzi wa darasa la saba shule ya msingi Higridge Joshua Proches alisema amefurahi kufika katika banda la JKCI kupata elimu na kujua nini kinachosababisha mtu kupata magonjwa ya moyo.
“Nimekuwa nikisikia watu wanaumwa moyo lakini sikuwa najua moyo unaumwa vipi na nini kinasababisha moyo kuumwa lakini baada ya kupata elimu kutoka kwa daktari nimejua”, alisema Proches