NA WALTER MGULUCHUMA,KATAVI
MSICHANA mmoja Mkazi wa Kijiji cha Kawanzinge Wilaya ya Mpanda mwenye umri wa miaka 14( jina linahifadhiwa) amefanyiwa kitendo cha kikatili cha kubakwa na mfungwa wa Gereza la Kalilankulukulu Wilaya ya Tanganyika wakati anatoka kupanda mpunga kwenye shamba la wazazi wake .
Tukio hilo limetokea Februari 29,2024 majira ya saa 11.00 jioni huko katika maeneo yanayopakana na mbuga za Gereza la Kalilankulukulu ambalo ni maarufu kwa kilimo cha Mpunga.
Kabla ya kufanya tukio hilo mfungwa huyo aliwatishia na kuwateka watoto waliokuwa na msichana huyo na kuwaweka chini ya ulinzi na na ndipo alipomchukua binti huyo na kumpeleka kwenye kichaka na kumfanyia unyama huo wa kumbaka
Mfungwa huyo kabla ya kutenda kosa hilo alikuwa akichunga ng’ombe katika eneo ambalo msichana huyo akiwa na wenzake walikuwa wakitembea kwa miguu wakati wakitoka shambani.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kawanzinge Emmanuel Machela amesema kuwa yeye alipata taarifa siku hiyo ya tukio majira ya saa tatu usiku kuwa kuna mtoto mwananchi wake amebakwa na mfungwa mmoja wa Gereza la Kalilankulukulu wakati akiwa anatoka shambani kupanda mpunga .
Amesema baada ya kuwa amepata taarifa hizo alipiga simu kwa Mkuu wa Gereza hilo msaidizi na kumweleza kuwa ni kweli wananchi wa Kijiji chake walikwenda kwenye Gereza hilo na kutoa taarifa kuwa mtoto huyo amebakwa hata hivyo aliwaruhusu warudi kijijini kwa kuwa ulikuwa haijathibitika kama amebakwa.
Baada ya kufika kijijini hapo wakiwa na kijana mmoja jina tunalo ambaye alikuwa na binti huyo ,katika maelezo yake alisema walipokuwa kwenye Gereza hilo na walipotoa taarifa mtoto huyo alipimwa kwenye Zahanati ya Gereza hilo na alipimwa na kuonekana amebakwa na alipewa dawa .
Naye Mwathirika wa tukio hilo amesema kuwa kabla ya kufanyiwa kitendo hicho na mfungwa huyo alimpinga ngwala na kisha alimfunga na sweta aliyokuwa nalo usoni na kisha alianza kumbaka licha ya kupiga kelele mfungwa huyo hakujali.
Alipomaliza kumfanyia ukatili huo alimuuliza mtoto huyo kuwa anakiasi gani cha fedha alichonacho ili amuachie na alimwambia kuwa anazo Sh.2000 mbazo alizichukua.
Baba mazazi wa mtoto huyo jina limehifadhiwa amesema kuwa binti yake ana kawaida ya kwenda kufanya vibarua kwenye mbuga za mpunga na huwa anaondoka asubuhi na kurudi jioni lakini siku hiyo hakurudi mapema hadi saa tatu usiku na kupata mashaka yeye na mkewe hali ambayo iliwafanya waende wakawatafute watoto wenzake walioondoka naye.
Ndipo walipoambiwa na mmoja wa watoto waliokuwa naye kuwa mwenzao amebakwa na wafungwa hali ambayo ilimlazimu akatoe taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijijini ambaye naye alimpigia msimu Kaimu Mkuu wa Gereza na alijibu kuwa malalamiko ya kubakwa kwa mtoto huyo yamefikishwa gerezani hapo.
Wakati wakiwa wamekaa kwa muda mrefu binti yake alifika kwa Mwenyekiti na aliwaeleza jinsi ambavyo alivyobakwa na ndipo walipoamua kwenda kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi cha Kata ya Kakese ambako nao waliwaambia waende moja kwa moja kwenye kituo cha polisi cha Wilaya ya Mpanda na baada ya kutoka kituo cha polisi cha wilaya walimpeleka kwenye hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda Dk.Limbu Mazoya amethibitisha kumpokea mtoto huyo kwenye hospitali ya Manispaa ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi imethibitika kuwa mtoto huyo amebakwa.
Kaimu Mkuu wa Gereza la Kalilankulukulu analiyetambulika kwa jina moja la Bosco amesema kuwa yeye hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo hadi mkuu wa Gereza alitolee ufafanuzi.