- MAPENZI dunia yake, tuyaache peke yake,
Tena yana bei yake, wala siashikeshike,
Mapenzi tusianike, kila mtu siri yake,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Kila mtu ana wake, akongaye moyo wake,
Na huyo usimtake, mwenyewe akasirike,
Atokako aibuke, makubwa na yafanyike,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Sitaki aadhirike, mwenzi wake umteke,
Pesa zako zitumike, kumfanya ageuke,
Mwenyewe yeye achoke, abaki asikitike,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Vipi wake umtake, wako kwako asitoke?
Wa kwake anunulike, wako abaki adeke?
Kwamba yeye aumbuke, na wewe ufaidike?
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Kwa Mungu ifahamike, mabaya yasifanyike.
Amri tuzikumbuke, tena sote tuzishike.
Asijetupiga teke, na kiama tuumbuke,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Kama mtu ana mke, halali ifahamike,
Nyumba na iheshimike, pande zote zihusike,
Wa tatu asiondoke, ya kwao yavurugike,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Huyo ni mume wa mke, na yeye afahamike,
Wala yeye asitoke, kwingine ashike shike,
Asifanye wasumbuke, mabinti na wanawake,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Hii na ifahamike, madhara tuyaepuke,
Mchepuko usikike, na kibano kikufike,
Wewe mochwari ufike, mwenyewe kitanzi kifike,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Kitaka yasikufike, kwingine siyapeleke,
Huko kwako uridhike, imani yako ushike,
Maadili yatukuke, kwa waume na wake,
Kuumizana mapenzi, athari hazipimiki. - Visasi visisikike, waume dhidi ya wake,
Ncha kali zisitoke, na maisha yatoweke,
Kesi zisiongezeke, familia situkuke,
Kuumiza mapenzi, athari hazipimiki.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602