NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umewaruhusu watoto pacha waliokuwa wameungana baada ya upasuaji wa kutenganishwa kufanikiwa na hali zao kutengamaa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuwaruhusu pacha hao waliozaliwa kwa nje wakiwa wameungana tumbo na kifua, ndani waliungana ini na mfupa wa kidari, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi, amesema uwekezaji wa kusomesha watalaamu, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi vya kisasa umeiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma zinazolingana na hadhi yake.
Aidha Dk.Janabi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutokana na uwekezaji uliofanyika hospitalini hapo ambao umewezesha huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi kufanyika ikiwemo upasuaji mkubwa wa kutenganisha watoto pacha.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Dk. Victor Ngota ameeleza kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao, ulichukua saa sita na kuhusisha jopo la wazawa lenye utaalam mchanganyiko wa hali ya juu wa madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, usingizi na ganzi, watalaam wa lishe pamoja na radiolojia.
“Tuliwapokea watoto hawa Machi 11,2023 wakiwa na jumla ya kilo nne hivyo tulianza mchakato wa kuwahusisha wataalamu ambao wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha ili kuweza kupata dira ya namna watakavyoishi mara baada ya kutenganishwa ambapo hadi wanatenganishwa walikua na kilo 16 sawa na kilo nane kwa kila mmoja” amefafanua Dk. Ngota.
Mzazi wa watoto hao Mariam Shabani, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, ameishukuru Serikali na watoa huduma wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi alivyohudumiwa katika kipindi chote alichokuwa hapo.






