- UTHUBUTU ni daraja, upate kufanikiwa,
Unakujengea hoja, kufanya yasofikiwa,
Unakwenda kama soja, sokubali kuzidiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Una madaraja mengi, kama ukiangaliwa,
Ya kawaida ni mengi, yafanywayo na wazawa,
Ila yale ya msingi, ndiyo yanayotugawa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Kuamua kuondoka, nyumbani na kuolewa,
Huo nao kwa hakika, uthubutu unakuwa,
Kibaki mpenda mama, shida kwako kuolewa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Samaria somo kwetu, yalofanywa nao hawa,
Njaa iliota kutu, jinsi walivyowangiwa,
Wakakosa hata utu, kula waliozaliwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Wakatokea wakoma, waliokuwa wakiwa,
Wakaona njaa noma, kwa kuwafanya kulewa,
Wangeamua kugoma, kwa jinsi walivyokuwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Wenyewe wakaazimu, athari wakizijuwa,
Wakajipanga kwa zamu, kusaka vinavyoliwa,
Adui hakufahamu, akajua kavamiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo ulipo.
- Walitoka masikini, kwa mali wakajaliwa,
Na hawakuona soni, taarifa wakazigawa,
Vyakula vingi sokoni, vikauzwa kama kawa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Lazima uazimie, ya kwamba hutachachawa,
Ucheke au ulie, sikubali kuzidiwa,
Utafanya ufikie, pale utakapokuwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Katika maisha yetu, sikubali kupaliwa,
Gumu liwe kama chatu, nalo laweza kuliwa,
Fanya mambo kimtutu, utayapata maziwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Tunaendelea mbele, kwa kugoma kuzidiwa,
Hata kuwe na kelele, tunaruka kama njiwa,
Hadi tufike kilele, huku tumefanikiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Moyo wa ajabu sana, kama vile una chawa,
Unabana zote zana, za kushinda kuvamiwa,
Ubakie kama jana, bila kitu kusifiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Kile wewe unataka, kufanya hutalemewa,
Kama ukikitamka, na mbinu kikaundiwa,
Nakuambia hakika, utaweza kama miwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Uthubutu ndio chanzo, cha kwako kufanikiwa,
Umeshapata mafunzo, usifanye kuzuiwa,
Hebu leo iwe mwanzo, ukitaka fanikiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Ukiwachunguza sana, kwa waliofanikiwa,
Kuthubutu kulifana, kama mechanganyikiwa,
Sasa hivi twawaona, kwamba wameshajaliwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Kuna usemi mzuri, wapaswa kusimuliwa,
Kwamba hadi kwenye dari, nako kwaweza fikiwa,
Bora mtu usikiri, kwamba umeshazidiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
- Mungu akupe akili, ya furusa kuelewa,
Nawe usikae tuli, ungojee kuchangiwa,
Kwa uamuzi mkali, njiayo hutapangiwa,
Bila wewe kuthubutu, utabaki hapo hapo.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602