NA MUNIR SHEMWETA, WANMM, ARUSHA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Mpango ameielekeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ile ya Ulinzi kwenda eneo la Oldonyosambu lilipo wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha kusikiliza na kutafuta suluhu ya changamoto ya wananchi na shamba la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Dk.Mpango ametoa maelekezo hayo Februari 10,2024 katika eneo la Oldonyosambu aliposimamishwa na wananchi barabarani wakitaka kusikikizwa changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo ikiwemo ya maji, barabara, umeme na shamba la Jeshi la Kujenga Taifa.
Katika kutoa majibu ya mgogoro huo. Dk Mpango aliwaambia wananchi hao kuwa, anawaelekeza mawaziri wa wizara hizo mbili kwenda eneo husika kwa lengo la kukutana na kuwasikiliza wananchi wa eneo hilo ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
“Naibu Waziri wa Ardhi, nakutaka urudi hapa ukiwa na mwenzako waziri wa ulinzi ulimalize jambo hili” alisema Dk.Mpango.
Awali wakati wa mkutano wa hadhara mara baada ya Makamu wa Rais Dk. Mpango kuzindua miradi ya umeme na kituo cha Afya Ketumbeine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda aliwaeleza wananchi wa Longido kuwa, wilaya hiyo kwa sasa iko shwari kwa kuwa changomoto pekee iliyopo katika eneo la ardhi ni ile ya mipaka ya wilaya aliyoieleza kuwa inafanyiwa kazi.
“Migongano hapa Longido imetulia na changamoto iliyopo ni ya mipaka ya wilaya na zipo timu zinafanyia kazi, niwashukuru wakuu wa wilaya kwa kazi kubwa ya kuwapa utulivu wananchi” alisema Pinda.
Aidha, Pinda ameonya wale wote wanaovamia maeneo ya ardhi na kuahidi wizara yake kushirikiana na wakuu wa wilaya katika kudhibiti uvamizi huo huku akitoa wito kwa watanzania kuwa, ardhi haiongezeki pamoja na idadi ya watu kuongezeka na kutaka busara kutumika katika kuitumia ardhi.
Katika ziara yake wilayani Longido Makamu wa Rais Dk. Mpango alizindua kituo cha afya Ketumbeine, Mradi wa REA pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari Wasichana ya Longido Samia Suluhu Hassan.