NA HAPPINESS SHAYO,DODOMA
WAZIEI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali iko katika mikakati ya kuhakikisha zao la asali linachangia kwenye pato la Taifa kwa kuongeza uzalishaji na uuzaji wa zao hilo nje ya nchi ili kuingiza fedha za kigeni.
Ameyasema hayo wakati wa kikao kati yake na Wabunge wa Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mara na Simiyu kilichofanyika leo Februari 10,2024 jijini Dodoma.
“Kwa sasa tunauza zao la asali kwa karibia asilimia tano lakini lengo letu ni isiwe chini ya asilimia 50 hivyo tutahakikisha tunazalisha asali nyingi zaidi” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema ili kufikia lengo hilo Serikali itafanya upembuzi katika tozo mbalimbali zinazohusiana na uzalishaji wa asali na ufugaji nyuki.
“Katika asali kuna bidhaa zaidi ya 15 lakini Kodi ya Ongezeko ya Thamani (VAT) imeondolewa katika vifaa vitano tu, hivyo tunaangalia vifaa vingine vinavyohusika katika mnyororo mzima wa uzalishaji asali VAT iondolewe ili kuongeza uzalishaji wa asali, mfano kwenye mavazi ya kurinia asali ,machujio na mengine” Kairuki amesema.
Sambamba na hilo, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutangaza utalii wa nyuki (Api-tourism) unaohusisha watalii kutembelea vijiji vya ufugaji nyuki na kushiriki katika zoezi zima la urinaji wa asali na kutumia nyuki kama tiba ya magonjwa (Apitherapy) kwa kudungwa na nyuki.
Aidha, amesema Wizara itazindua mkakati wa ufugaji nyuki wa miaka 10 (2024-2034) mwezi Mei mwaka huu Jijini Dodoma ambapo itaangalia sekta nzima ya ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali.
Wakati huohuo, Kairuki amesema Serikali inaangalia namna ya kuboresha mazao yatokanayo na misitu kwa kupitia upya tozo na kodi ambazo hazitakiwi, kuangalia mitambo itakayosaidia zaidi kwenye uchakataji wa mbao na kuongeza thamani katika mazao ya mbao.
Akizungumzia kuhusu utangazaji utalii Kairuki amesema Serikali itaendelea kutangaza, kubuni na kuvumbua maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii.
Waziri Kairuki amehitimisha kwa kuahidi kufanyia kazi mapendekezo ya wabunge ikiwa ni pamoja na suala la malipo ya kifuta jasho/machozi ,fedha za ujirani mwema (Community Social Responsibility) na kushughulikia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb), baadhi ya Wabunge wa Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mara na Simiyu pamoja na Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bodi ya Utalii Tanzania, Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)