NA MUNIR SHEMWETA, WANMM,MPIMBWE
WAKAZI wa jimbo la Kavuu katika eneo la Mwamapuli katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi wamekosa maswali ya kumuuliza Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi Geophrey Pinda kutokana na kukamilisha asilimia kubwa ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka 2020.
‘’Hivi mna kero hapa kweli, kuna mtu ana jambo la kumuuliza Mbunge kuhusu alichokuwa anasema wakati wa kampeni? na kama yupo anyanyue mkono na aseme’’ alihoji mPinda.
Hayo yamebainika Februari 3,2024 wakati Mbunge wa Jimbo hilo alipokwenda kuwafariji wananchi waliopatwa na ugonjwa wa kipindupindu katika eneo la Mwamapuli halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Akiwa katika eneo hilo, Pinda amewataka wananchi wa Mwamapuli kufanya kazi kwa bidii na kuweka wazi kuwa inapoelezwa kuwa eneo la Mwamapuli lina changamoto aniatafuta kwa kuwa kazi kubwa ameifanya kulihudumia jimbo la Kavuu.
‘’Wana Mwamapuli ukisema kuna changamoto naitafuta usiku na mchana tulikuwa na changamoto nzito lakini tumeziamua na zimebaki za kawaida tu’’ alisema Pinda.
Amewaomba wananchi wa jimbo hilo kutorudi nyuma katika kufanya kazi na kuwaeleza kuwa jimbo la Kavuu lipo juu hususan katika uzalishaji mazao kama vile mahindi na mpunga huku akiwaeleza wana jimnbo hilo kuisikia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kazi iendelee.
Kwa mujibu wa Pinda. Kauli ya kazi iendelee ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inajidhihirisha kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa miundombinu ya barabara, daraja pamoja na uboreshaji huduma za afya kama vile ujenzi wa vituo vya afya, zahanati sambamba na upatikanaji wa huduma ya maji.
Akigeukia ugonjwa wa kipindupindu uliwapata baadhi ya wananchi wa Mwamapuli, Pinda aliwataka wananchi wa eneo hilo kuanza juhudi za kutokomeza ugonjwa huo kwa kuwa wasafi pamoja na kuhakikisha kila nyumba inakuwa na choo.
‘’Nataka ugonjwa huu uondoke kwa siku moja kwa kuhakikisha mnakuwa wasafi na mnachemsha maji, mnaniahidi kuondoa kipindu pindu ndani ya siku moja?’’ alisema Pinda
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Pinda alikuwa jimboni kwake kwa ziara ya siku moja ambapo alifanya shughuli mbalimbali kama vile ukaguzi wa barabara ya kilomita 70 Kibaoni – Sitalike, kukabidhi magari ya wagonjwa pamoja na kuwafariji wananchi waliopatwa na ugonjwa wa kipiundupindu kwenye eneo la Mwamapuli.