NA TERESIA MHAGAMA, DODOMA
KATIKA jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa
uhakika, Serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa
Gridi katika Mkoa wa Rukwa kupitia mradi wa TAZA ulioanza kutekelezwa
mwezi Novemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026.
Hayo yameelezwa leo February Mosi,2024 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida
Khenani aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya
upatikanaji umeme wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO inaendelea kufanya maboresho ya
miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo
na kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.
Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini amesema kuwa, upungufu wa
umeme unaendelea kupungua akitaja takwimu kuwa, upungufu umepungua
kutoka megawati 400 hadi 144 kwa siku ya leo.
Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili
kuboresha hali ya upatikanaji umeme nchini akitolea mfano utekelezaji
wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao inatarajiwa kuwa,
katika mwezi wa Pili Kuelekea mwezi wa Tatu mwaka huu, utaanza
kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.
Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi mkoani
Katavi ambapo ameeleza kuwa, tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa
na kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo,
nguvu sasa inawekwa zaidi katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme
kwenda mkoani humo.