NA FARIDA RAMADHANI,WF,DODOMA
TANZANIA na Global Fund zimesaini Mikataba minne ya misaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 606.9 (sawa na zaidi ya Sh. Trilioni 1.4) kwa ajili ya kupambana na maradhi ya Ukimwi Kifua Kikuu, Malaria na Uimarishaji wa mifumo ya afya nchini.
Mikataba hiyo imesainiwa Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Global Fund- Afrika, Linden Morrison.
Nchemba alisema msaada kutoka Global Fund umepangwa kutekelezwa kwa miaka mitatu ambapo mpaka sasa Tanzania imepokea misaada kwa vipindi vinne ambavyo ni Julai 2012 – Desemba 2014, Julai 2015 – Desemba 2017, Januari 2018 – Desemba 2022 na Januari 2021 -Desemba 2023.
“Miradi inayotekelezwa kupitia msaada wa Global Fund kwa kipindi cha kuanzia Januari 2024 hadi Desemba 2026 itatekelezwa na Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Wizara ya Fedha inaendelea kuwa Mpokeaji Mkuu wa Sekta ya Umma na Management and Development for Health (MDH) ni Mpokeaji Mkuu wa pili kwa Sekta Binafsi”, amebainisha Nchemba.
Aidha, aliishukuru Global Fund kwa kuendelea kuisaidia Tanzania na kubainisha kuwa misaada hiyo inatokana na juhudi mbalimbali anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya nchi iaminike Kimataifa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema watatumia fedha hizo kikamilifu katika kuimarisha kinga dhidi ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu ambapo asilimia 75 ya fedha hizo wamezielekeza kwenye bidhaa za afya.
“Kwa upande wa UKIMWI tutahakikisha takribani Watanzania milioni 1.7 ambao wanamaambukizi wanapata dawa za kufubaza makali ya UKIMWI au ARV’s kila mwaka”, alisema Mwalimu.
Alisema msaada uliotolewa ni kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026 na inalenga kuboresha mifumo ya maabara, mitungi ya Oksijeni, kuboresha mazingira ya watumishi wa afya na kuimarisha mnyororo wa thamani.
Aidha Morrison alisema kuwa msaada huo unakwenda sambamba na vipaumbele vya Serikali ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya Afya nchini.





Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha kusimamia utekelezaji wa
programu iliyoishia Desemba 2023 ambapo ilipata matokeo mazuri ya matumizi ya fedha kutoka mfuko huo katika masuala yakupunguza maambukizi ya HIV, Maralia na kifua kikuu.