NA TERESIA MHAGAMA, DODOMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko pamoja
na Waziri wa Masuala ya Nishati wa Zambia, Peter Kapala wamefanya kikao kilicholenga kujadili nia ya Serikali ya Tanzania na
Zambia kuanza ujenzi wa bomba la inchi 24 la kusafirisha mafuta safi
kutoka Tanzania kwenda Zambia.
Kikao hicho kimefanyika Januari 29 , 2024 jijini Dodoma na
kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Makatibu
Wakuu wa Wizara za Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (Tanzania) na
Dk. Chisangano Zyambo (Zambia) pamoja na watendaji mbalimbali kutoka
Wizara hizo na Mashirika yanayosimamia Mafuta.
Dk Biteko amesema, majadiliano hayo ya Mawaziri yanatokana na ziara
ya Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini
Zambia mwezi Oktoba mwaka 2023 ambapo katika mazungumzo yake na Rais
wa Zambia, Hakainde Hichilema walijadiliana kuhusu kuongeza
uwekezaji kwenye Bomba la Mafuta la TAZAMA kwani bomba hilo kwa sasa
halikidhi mahitaji kutokana na kuwa na ukubwa wa inchi 12.
“Kulingana na maendeleo makubwa katika nchi zetu mbili, mahitaji ya
mafuta yamekuwa makubwa ndio maana inabidi kujenga bomba jingine jipya
kubwa ambalo litasafirisha mafuta kutoka Tanzania kwani kuna Bandari,
bomba hili litakalojengwa pembeni ya Bomba la Mafuta la TAZAMA
litasafirisha mafuta pia kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania na hivyo
kupunguza gharama za usafirishaji na kuwapatia wananchi mafuta ya
gharama nafuu.” amesema Dk Biteko.
Ameeleza kuwa, bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,710 na
uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 na kusisitiza kuwa, kwa
uwekezaji huo kunahitajika umakini kwenye utekelezaji wake na bila
kuuchelewesha.
Ameongeza kuwa, bomba litakuwa na matoleo ya Mafuta katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo Morogoro, Makambako, Mbeya na Songwe na
kupunguza suala la mikoa hiyo kutegemea kupakua mafuta jijini Dar es
salaam pekee.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Timu ya Wataalam wamajadiliano inaanza kazi
leo na hii ikiwa ni msukumo ambao Marais wa nchi zote mbili wamekuwa
wakiutoa ili kutekeleza mradi huo.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania, ipo tayari kutekeleza mradi huo
wa kimkakati na hii ikizidi kuonesha uhusiano mzuri uliopo kati ya
nchi hizi mbili ambao umepelekea utekelezaji wa miradi mbalimbali
ikiwmemo wa bomba la TAZAMA na mradi wa usafirishaji umeme kutoka
Tanzania kwenda Zambia wa kV 400.
Kwa upande wake, Waziri wa Masuala ya Nishati wa Zambia,
Kapala amesema kuwa, nchi hiyo inauhitaji sana mradi huo na Rais wa
nchi hiyo anaupa msukumo na anatarajia kwamba kazi ya utekelezaji
itafanyika kwa kasi na umakini ikitarajiwa kuwa mradi ukamilike kwa
muda wa miaka miwili.
Ameeleza kuwa, kampuni nyingi zimeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili
ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo ametanabaisha kuwa nia za
makampuni hayo zitafanyiwa tathmini na wataalam ili kupata kampuni
bora.
Ameongeza kuwa, mahitaji ya mafuta nchini Zambia yanazidi kuongezeka
kutokana na kukua kwa shughuli za maendeleo nchini humo ikiwemo
uanzishwaji wa migodi ya madini ya shaba hivyo Serikali ya Zambia ipo
tayari kutekeleza mradi huo.