- HII ni elimu nzuri, tusije kuipuuza,
Raha za muda ni nzuri, japo mbele zaunguza,
Hivi nakupa habari, usije ukapuuza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Vijaavyo kirahisi, bila jasho kuchomoza,
Vikufanyavyo uhisi, starehe waongeza,
Unategwa na kirusi, kujitoa hutaweza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Mungu kakupa ujuzi, uweze kujiongeza,
Wewe hufanyii kazi, wakaa wajilegeza,
Kwako huo ni ulozi, mwenyewe wajichuuza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Ukidharau talanta, ulopewa na Muweza,
Na hata ile talanta, ulivyojiendeleza,
Utapoteza talanta, nafasi ya kujieneza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Ujuzi wako uhuru, kipato kukiongeza,
Huo unakupa nuru, pale palipo na giza,
Ni lulu usikufuru, hiyo ukatelekeza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Kuyafanya maamuzi, yawezayo kukujaza,
Usilale usingizi, muda ukapitiliza,
Amua fanyia kazi, bila muda kupoteza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Ukifanya maamuzi, kujiburuza buruza,
Kwako ni maangamizi, vile utavyopoteza,
Amka fanyia kazi, mwenyewe kijiongoza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Hebu angalia watu, na jaribu kuchunguza,
Wengi tawaona watu, na hata kuwapongeza,
Sababu ya uthubutu, ulowafanya kuweza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Huko huko kuna watu, ambao wajilegeza,
Maisha yao ni butu, hakuna cha kupongeza,
Kwenda kufyeka msitu, kwao ni kujiumiza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani. - Ili weze lima shamba, machaka ni kupunguza,
Mikono yaweza vimba, ndivyo unajisogeza,
Utavuna kule shamba, kama hutajilegeza,
Ni lazima kupambana, kupata vyenye thamani.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602