NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kuwa imemkamata mtuhumiwa wa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina ya Cocaine ( jina linahifadhiwa hadi pale atapofikishwa mahakamani)nchini pamoja na kukamata jumla ya gramu 692.336 za dawa hizo zinazowahusisha watuhumiwa wanne.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa dawa hizo alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu alikamatwa katika eneo la Boko wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na washirika wake watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 25,2024 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema washiriki watatu na mfanyabiashara huyo kati yao wawili walikamatwa jijini Dar es Salaam na mmoja alikamatwa katika kijiji cha Shamwengo wilaya ya Mbeya vijijini mkoani Mbeya.
Amesema katika utafiti wao wamebaini kuwa wafanyabiashara wa mtandao wa cocaine wamekuwa wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia watu ambao humeza dawa hizo tumboni au kuweka kwenye maungo mengine ya mwili.
“Mfanyabiashara huyu aliyekamatwa ana mtandao mkubwa wa wabebaji maarufu kama punda kutoka nchi mbalimbali ambao huwatumia kusafirisha dawa hizo kwa njia ya kumeza, hivyo makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka.
“Dawa ya kulevya aina ya Cocaine huzalishwa kwa wingi katika bara la Amerika ya Kusini na husafirishwa kwa njia ya anga na wabebaji (punda) huzimeza zikiwa katika mfumo wa pipi ambapo kwa mara moja mtu mmoja hubeba kuanzia gramu 300 hadi 1200 na baadhi yao huweza kubeba hadi gramu 2000 kwa wakati mmoja,” amesema Kamishna Lyimo
Aidha amesema dawa hiyo ya kulevya ya cocaine huzalishwa kutoka kwenye mmea wa Coca unaaojulikana kitaalam kama Erythroxylum coca (coca Plant) ambao hulimwa zaidi katika nchi za Bolivia, Peru na Colombia zilizopo Amerika ya Kusini.
“Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji kwani huathiri utendaji wa mfumo wa fahamu, husababisha kukosa usingizi, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi na vifo vya ghafla, aidha Cocaine inaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili, ukatili, vurugu, kukosa utulivu na hata mtumiaji kutaka kujiua,” amesema Lyimo
Amesisitiza kuwa dawa hiyo ya Cocaine husababisha uraibu wa haraka na utegemezi na hivyo kuwa vigumu kwa mtumiaji kuiacha