NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kuwa itafanya oparesheni kali za nchi kavu na baharini kwa mwaka huu ili kuweza kusaka dawa za kulevya nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 25,2024 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kuwa oparesheni za nchi kavu zitahusisha mashamba ya dawa za kulevya, kwenye mipaka, maeneo ya mijini kwenye vijiwe vya usambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.
Lyimo amesema kwa upande wa baharini oparesheni zitahusisha fukwe na katikati ya bahari.
“Operesheni hii itahusisha pia maeneo yote wanayouza shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ambapowale wotè watakaòbainika kutumia dawa hizo kupitia shisha watachukuliwa hatua kali za kisheria, Vilevile oparesheni hii itahusisha wauzaji wanaokiuka taratibu za uuzaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu,” amesema
Aidha Lyimo ametoa onyo kwa wote watakaoendelea kujihusisha na uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha kwani serikali imeendelea kuiwezesha mamlaka hiyo kwa kununua vifaa vya kisasa na mafunzo kwa watumishi ili kuwajengea ujasiri na weledi katika kutekeleza oparesheni kwa ufanisi mkubwa.
“Hivyo kwa wale wote watakaoendelea na kilimo cha bangi, mirungi na biashara ya dawa za kulevya za viwandani watashughulikiwa ipasavyo, ” amesema Kamishna Lyimo na kuongeza
“Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wote wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa salama kwa kupiga simu namba ya bure 119 na taarifa zitapokelewakwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi,”